**************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Wachukuzi wameishukuru Serikali iliyopo madarakani inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kusimama pamoja nao na kuhakikisha wanalipwa fedha zao ambazo walikosa matarajio lini watazipata.
Hayo yamebainishwa na Wachukuzi wa Chama cha msingi (Amcos) cha Kitama shuleni kilichopo kata ya Kitama ambao fedha zao zilienda kulipa madeni ya Amcos badala ya kulipwa haki zao na ndipo Serikali ikaingilia kati na kuhakikisha wanalipwa fedha zao.
“Tunaishukuru Serikali ya Rais Magufuli, tunamshukuru sana Afisa Tarafa wetu kwa kusimama pamoja nasi kuhakikisha tunalipwa fedha zetu. Tunamshukuru sana Gavana Shilatu.” Alisema mmoja wa Wachukuzi.
Akizungumza na Mwandishi wetu, Afisa Tarafa Mihambwe *Ndugu Emmanuel Shilatu* alisema Serikali ya awamu ya 5 inasimama na Watu wanyonge ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipoteza haki zao pasipo Mtetezi.
“Niliposikia fedha za Wachukuzi zimeenda kulipa madeni ya chama cha Kitama shuleni nilikasirika sana, nikawaita viongozi pamoja na Wachukuzi mezani na hatimaye mwafaka ukapatikana na Amcos wamekubali kulipa fedha zao mapema iwezekanavyo. Nitasimamia hili mpaka ukamilifu wake.” Alisisitiza Gavana Shilatu.
Wachukuzi wa Kitama shuleni wanaidai Amcos hiyo fedha za msimu 2018/2019 ambazo sasa wamepata mwangaza wa malipo ya fedha zao.
Kikao hicho kilihudhuliwa na Afisa Tarafa Mihambwe Gavana Shilatu, Mwenyekiti wa Serikali Kijiji cha Kitama Shuleni, Mtendaji Kijijini cha Kitama Shuleni, Uongozi na Bodi nzima ya Kitama Shuleni Amcos pamoja na Wachukuzi wenye madai na Amcos hiyo.