***************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Bw. Geoffrey Mwangulumbi pamoja na Mwekahazina wa Manispaa hiyo, Bw. Pascal Makoye kuwa anawataka wabadilike na waache kugombana na badala yake watekeleze majukumu yao ipasavyo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bibi Zainab Telack azisimamishe kazi kampuni zote zilizopewa zabuni ya kukusanya mapato katika Manispaa hiyo kwa kuwa zimeshindwa kufanya kazi vizuri na zina madeni.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Ijumaa, Agosti 9, 2019) wakati alipozindua nyumba 10 za Askari Polisi katika Manispaa ya Shinyanga eneo la Kambarage. Mradi huo umetokana na fedha kiasi cha sh. milioni 225 zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli.
Amesema viongozi hao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ikiwemo kusimamia kikamilifu zoezi la ukusanyaji wa mapato na kutoa kazi hiyo kwa kampuni zisizokuwa na uwezo. Amesema mwaka jana walikadiria kukusanya sh. milioni 800 na badala yake walikusanya sh. milioni 500.
Waziri Mkuu amesema Manispaa hiyo haiwezi kusonga mbele kimaendeleo iwapo viongozi wake hawaelewani wanagombana kila siku. “Mkurugenzi na wenzako nawaonya kwa mara ya mwisho badilikeni na hakikisheni mnatekeleza majukumu yenu ipasavyo yakiwemo ya ukusanyaji wa mapato.”
Akizungumzia kuhusu nyumba za Askari Polisi, Waziri Mkuu amesema lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni kuhakikisha askari wanaishi katika mazingira mazuri yatakayowawezesha kutekeleza vizuri majukumu yao. “Ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao lazima wawe na makazi mazuri”.
Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa askari waliopewa funguo kwa ajili ya kuishi katika nyumba hizo wahakikishe wanazitunza vizuri na hata inapotokea wamehamishiwa kwenda katika vituo vingine, wale watakaohamia wakute nyumba hizo zikiwa katika mazingira mazuri.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa nyumba hizo ni endelevu, ambapo pia amezitaka idara mbalimbali za Serikali ziendelee na mchakato wa ujenzi wa nyumba zake kwani wakiwa na nyumba nyingi itasaidia kupunguza idadi kubwa ya askari wanaoishi uraiani.
Awali, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao alisema awali fedha zilizotolewa zilikuwa zijenge nyumba tisa za vyumba viwili lakini kutokana na ubunifu waliweza kuboresha mradi huo kwa kuongeza nyumba moja sambamba na kuongeza chumba kimoja, hivyo kuufanya mradi huo kuwa na nyumba 10 zenye vyumba vitatu vya kulala.
Pia alimshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa upendo wake mkubwa kwa Jeshi la Polisi Tanzania kwa kulipatia fedha za kuboresha makazi ya askari. Mradi huo umekamilika kwa gharama ya sh. milioni 278, 565, 500 wastani wa gharama za ujenzi kwa nyumba moja ni sh. milioni 27, 856, 550. Alisema kiasi cha nyongeza cha sh. milioni 53, 565,500 zilitolewa na wadau mbalimbali.