Shirika la Wakala wa Meli Nchini (TASAC) imewataka wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona kuna bandari bubu au usafiri wa vyombo vya usafiri ambavyo havijasajiliwa kwenye maeneo yao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Shirika, Bw Mathias Mhembe leo kwenye kilele cha sikuku ya wakulima (Nanenane) jijini Dodoma.
Mhembe amesema TASAC inafanya kazi kwa karibu na mamlaka zingine ikiwemo Polisi hivyo wananchi wanapoona uwepo wa bandari bubu ni vema wakatoa taarifa kwenye Ofisi za Kata ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
” TASAC tumejikita katika udhibiti wa huduma za bandari na usafiri wa Meli, lengo letu ni kutokomeza bandari bubu ambazo zinainyima Serikali mapato pamoja na kuhakikisha pia usalama wa wananchi wanaotumia usafiri wa Majini unakuepo,” amesema Mhembe.
Amesema kazi nyingine zinazofanywa na Shirika hilo ni pamoja na udhibiti ulinzi, usalama wa vyombo vya usafiri majini, udhibiti usimamizi na utunzaji wa mazingira bandarini pamoja na usimamizi wa huduma za biashara za meli.
” Shirika lilianzishwa mahususi kudhibiti vyombo vya majini, kazi yetu ni kufanya ukaguzi mara kwa mara ili kuangalia uimara na ubora wa vyombo vya usafiri lengo likiwa ni kuhakikisha usalama wa abiria, lakini pia tunatoa elimu ya uokoaji pindi linapotokea tatizo na kukagua pia vifaa vya uokoaji kama vipo,” amesema Bw Mhembe.
Aidha amesema ni makosa kisheria kufanya biashara ya usafiri wa majini bila kusajiliwa na kutoa rai kwa yeyote anayetaka kufanya biashara ya usafiri wa majini kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kusajili.