************
Msanii Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platnumz leo amefanya ziara ya kuhamasisha utalii wa ndani kwa kutembelea mashamba ya zabibu Jijini Dodoma na kuwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya Utalii ndani ya nchi ili kukuza sekta hiyo hapa nchini.
Diamond ameyasema hayo leo Nkhulabi,Kata ya Mpunguzi alipotembelea mashamba ya zabibu na kujionea shughuli za uzalishaji mvinyo katika kiwanda cha usindikaji mvinyo cha Dane Holdings Co.Ltd kinachomilikiwa na Eng.Danford Semwenda.
“Najisikia furaha kutangaza mema ya nchi yangu na hasa zabibu za Dodoma kwa kuwa ndio eneo lenye zabibu zenye ubora wa juu sana duniani.Nitatumia sanaa yangu kuhakikisha nashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli kwa kuifanya dunia kujua utajiri wa vivutio vya utalii Mungu alivyotujalia”Alisema Mavunde
Aidha Wabunge Mh Livingstone Lusinde na Mh Anthony Mavunde wamewataka wananchi wa Dodoma kulichangamkia zao la zabibu kwa kulima kwa wingi kwa kuwa muda sio mrefu mahitaji ya zabibu yatakuwa makubwa hasa kutokana na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli kwa kushusha tozo ya mchuzi wa zabibu kutoka Tsh 3315 mpaka Tsh 450 na kumshukuru Diamond kwa kuamua kuitangaza zabibu ya Dodoma kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania((TTB)
Akitoa maelezo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Mkuu wa Wilaya wa Bahi Mh Mwanahamis Mukunda amempongeza Msanii Diamond kwa kuwa mfano kwa wasanii wengine katika kutangaza vivutio vya utalii nchini na kumuomba mwanamuziki huyo kushirikiana na uongozi wa serikali ya Mkoa wa Dodoma kwa kulitangaza Tamasha la Mvinyo (Wine Festival 2019) kwa kuwa mkoa wa Dodoma umejipanga kurudisha heshima ya zao la zabibu.