Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyeinua
mkono) akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Sira Ubwa Mamboya (aliyeketi mbele) alipowasili ofisini
kwake, Dodoma kwenye ziara ya kutembelea taasisi za Mawasiliano
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyevaa shari
nyeupe katikati) akiwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Sira Ubwa Mamboya (wa kwanza kushoto kwake)
walipotembelea mnara wa mawasiliano uliojengwa na UCSAF kijiji cha Makanda, Bahi,
Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Dkt. Sira Ubwa Mamboya (aliyevaa ushungi)akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa
Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi. Justina Mashiba (hayupo pichani) walipotembelea
mnara wa mawasiliano uliojengwa na UCSAF kijiji cha Makanda, Bahi, Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Dkt. Sira Ubwa Mamboya akizungumza ofisini kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto)wakati wa ziara yake ya
kutembelea taasisi za Mawasiliano, Dodoma.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi. Justina Mashiba (aliyesimama)akitoa taarifa ya Mfuko huo kwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Sira Ubwa Mamboya (aliyevaa ushungi)wakati wa ziara yake. Pembeni kwake ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye.
***********
Na Mwandishi Wetu,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Dodoma, 8 Julai 2019 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) nchini kwa kuipa kipaumbele miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mfuko huo kwa upande wa Zanzibar.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Sira Ubwa Mamboya alipotembelea Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) jijini Dodoma akiongozana na mwenyeji wake
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Atashasta Nditiye (Mb) pamoja na
ujumbe wake kutoka katika Wizara anayoiongoza.
Akizungumza na Uongozi wa Mfuko huo, alisema UCSAF imetoa kipaumbele kwa
miradi mikubwa mitatu ambayo itaongeza maendeleo ya matumizi ya TEHAMA Visiwani Zanzibar.
“Nawashukuru sana kwa kujenga vituo vya mawasiliano Zanzibar na minara ya
mawasiliano ambapo inawawezesha wananchi kutuia huduma za mawasiliano kwa
shughuli za kijamii na kiuchumi visiwani humo. Aidha, ameongeza kuwa amefurahishwa na mkakati wa kuwahamasisha wasichana kujitokeza na kupata mafunzo katika programu ya Wasichana na TEHAMA, “Hii itawafanya wasichana wa Zanzibar kuwa mstari wa mbele kutumia TEHAMA na kuingia katika mfumo wa Elimu ya TEHAMA,”amesema.
Pia, ameishukuru na kuipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji katika kupanga na kutekeleza mipango mbali mbali inayohusu Sekta ya Mawasiliano kwa kuwa mawasiliano ni suala la Muungano.
Naye Mhe. Nditiye (Mb) alisema kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
imefarijika sana kuupokea ujumbe wa Mheshimiwa Dk. Mamboya ambao umekuja
Tanzania Bara kujifunza na kubadilishana uzoefu kuendana na utendaji kazi wa kila siku wa taasisi za Mawasiliano kwani mawasiliano ni suala la Muungano. Nditiye alimhakikishia Mhe. Dk. Mamboya kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itahakikisha inaendelea kutoa ushirikiano kwa SMZ kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ili kuendelea kutekeleza majukumu na kuhudumia wananchi katika nyanja ya mawasiliano.
Wakati akitoa taarifa ya Wizara kwa ugeni huo, Nditiye alisema kuwa tayari Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imejenga na kufikisha Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo Unguja inaunganishwa na Mkongo huo kupitia mkongo wa baharini uliopo kwenye waya wa umeme kutoka Dar es Salaam na Pemba imeunganishwa kutoka Tanga. Pia, aliongeza kuwa vituo kumi vya TEHAMA vimejengwa na UCSAF kwa gharama ya shilingi milioni 754.8 ambapo vituo sita vimejengwa Unguja na vituo vine vimejengwa Pemba na tayari kila kituo kimepewa kompyuta saba na printa moja kutoka UCSAF.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF aliishukuru Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ya SMZ kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mfuko wakati wa kutekeleza miradi ya TEHAMA kwa upande wa Zanzibar. Alisema Wizara hiyo imekuwa karibu na Mfuko jambo ambalo limepelekea mafanikio ya miradi ya TEHAMA visiwani humo.
Akielezea utekelezaji wa miradi ya TEHAMA Visiwani Zanzibar, Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bibi Justina Mashiba amesema, jumla ya wasichana 40 kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamepewa mafunzo ya utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA kutoka mikoa ya Kaskazini Pemba na Mjini Magharibi. Aidha alisema Mfuko umetoa vifaa vya TEHAMA kwa shule 16 Zanzibar, uboreshaji wa mawasiliano kwenye Kata 10 zenye vijiji 18 Zanzibar.