Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akikagua Mradi wa Maji wa Gamasara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa kwenye kituo kimojawapo cha kuchotea maji cha Mradi wa Maji wa Mika katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akipampu maji kwenye moja ya kisima cha maji katika Kijiji cha Gamasara ambacho kinatumia pampu ya maji ya bei nafuu iliyotengenezwa na mhitimu wa Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), James Ryoba, Mhandisi wa Maji na Umwagiliaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiwa kwenye Mradi wa Maji wa Sirari pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Kabeho (wa tatu kulia) na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), Mhandisi Robert Lupoja (wa mwisho kulia) wilayani Tarime, mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kushoto) akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Kabeho alipokuwa ziarani katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime akikagua miradi ya maji, mkoani Mara.
Ujenzi wa tenki la maji la Mradi wa Maji wa Gamasara uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani, Mara.
……………………
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameelekeza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuvunja mkataba na Mkandarasi wa Kampuni ya Kumba Quality Ltd inayotekeleza kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Gamasara, mkoani Mara.
Naibu Waziri Aweso amechukua maamuzi hayo baada ya kukagua mradi na kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Gamasara ulioanza mwaka 2018 na Serikali imeshamlipa mkandarasi kiasi cha Shilingi milioni 50 lakini mpaka kufikia mwezi Agosti, 2019 utekelezaji wake ni asilimia 20 na mkandarasi akiwa ametoweka site bila taarifa yoyote.
Naibu Waziri Aweso amewataka wataalam wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Mara na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kusimamia ujenzi huo na kukamilisha kazi zilizobaki.
Aidha, Naibu Waziri Aweso amekagua moja ya kisima cha maji katika Kijiji cha Gamasara ambacho kinatumia pampu ya maji ya bei nafuu iliyotengenezwa na mhitimu wa Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), James Ryoba, Mhandisi wa Maji na Umwagiliaji.
Mhe. Aweso amempongeza James Ryoba kwa kuonyesha ubunifu wa kutengeneza pampu ya maji kwa gharama nafuu kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Tarime.
Amesema Mhandisi Ryoba ni mfano wa kuigwa kwa vijana wote waliohitimu elimu za vyuo nchini kwa kutumia taaluma zao kuwa wabunifu, baada ya kupoteza muda kwa kusubiri kuajiriwa wakati wakiwa na uwezo wa kujiajiri.
Naibu Waziri Aweso amemuelekeza Mkurugenzi wa MUWASA, Mhandisi Robert Lupoja kumpa ajira ya muda kwenye mamlaka hiyo, wakati unafanyika utaratibu wa kumtafutia ajira ya kudumu.