Mbunge wa Viti maalum anayewakilisha vijana Mhe Mariam Ditopile amekabidhi vitendea kazi zikiwemo Kompyuta zenye thamani ya Shilingu Milioni mbili pamoja na fedha taslimu Shilingi Laki Sita kwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar Es Salaam.
Mhe Ditopile amekabidhi vitu hivyo wakati wa ufunguzi was Baraza la Vijana ambapo pia aliwaasa UVCCM kujitokeza hadharani kujibu porojo ambazo zimekua zikielekezwa kwa Chama na Serikali.
Amewataka vijana wa CCM kuyaeneza mazuri ambayo yamekua yakifanywa na Serikali ya Rais Magufuli bila kuona aibu na kuwasihi kusimamia mstari katika kuijenga Tanzania ya viwanda kwa vitendo na siyo maneno.
” Niwasiihi vijana wenzangu kuwa mstari wa mbele kuyasema na kuyatangaza hadharani yale yote yanayofanywa na serikali ya CCM katika kutekeleza ilani yake ya mwaka 2015 ambao ndio msahafu unaotuongoza ndani ya miaka hii mitano.
Na tunaposema tuunge mkono juhudi za Mh Rais Magufuli katika hizi zama za kuchapa kazi kama kauli mbiu yake inavyosema ya hapa kazi tu wananchi nao wajue ni kazi kweli kwa sababu hata sisi vijana tutaonekana kweli tunaitekeleza Ilani kwa kufanya kazi,” amesema Mhe Ditopile.
Aidha amewapongeza UVCCM Dar Es Salaam kwa kuwa waasisi wa KIJANI na kuongeza kuwa hivi sasa nchi nzima kampeni hiyo imekua kubwa na imezidi kukiimarisha Chama hicho kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
” Nawapongeza kwa kuwa waasisi wa kampeni ya Kijani ambayo imefanikiwa, ila niwanasihi juhudi hizi kubwa zisiishie kwenye matamasha tu bali ni lazima ziwe chachu ya kuhakikisha ushindi mnono kwa Chama chety katika chaguzi zilizo mbele yetu,” amesema Mhe Ditopile.