Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kushoto), akikata utepe kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika Kijiji cha Mwelani, Kata ya Mganza wilayani Chato, Mkoa wa Geita. Wengine katika picha ni viongozi katika Kata hiyo.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia) akigawa vifaa vya UMETA kwa wananchi wa Kijiji cha Mwelani wilayani Chato ambacho kitawawezesha kuunganishwa na umeme bila kuingia gharama za wiring.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia) akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mwelani wilayani Chato kabla ya kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho.
Wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakiwa katika Mkutano wa Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na wananchi wa Kijiji cha Mwelani wilayani Chato.
…………………….
Teresia Mhagama na Hafsa Omar, Geita
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameendelea kusisitiza utekelezaji wa agizo alilolitoa la wananchi vijijini kutotozwa gharama ya nguzo pale wanahitaji kuunganishiwa umeme.
Dkt. Kalemani alisema hayo tarehe 7 Agosti, 2019, wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mwelani, Kata ya Mganza wilayani Chato mkoani Geita kabla ya kuwasha umeme rasmi katika Kijiji hicho.
“ Kuna baadhi ya wananchi wanalalamika kuwa wakienda kulipia huduma ya umeme ofisi za TANESCO au kwa Wakandarasi, wanaambiwa kuwa walipie nguzo, hili suala nimeshalikataza nchi nzima,” alisema Dkt Kalemani.
Vilevile Dkt. Kalemani aliagiza kuwa, wananchi wasikataliwe kutoa malipo pale wanapotaka huduma ya umeme kwa kisingizio cha kutokuwepo kwa vifaa kwani suala hilo limekuwa kama kigezo cha kuwacheleweshea huduma wananchi.
Akizungumza na wananchi katika Kijiji hicho aliwahakikishia kuwa, vitongoji vyote vinne vilivyopo kwenye Kata hiyo vitapata umeme.
Aidha, alitoa agizo kwa Meneja wa TANESCO Wilaya ya Chato kufungua ofisi ndogo ya TANESCO kwenye Kata ya Mganza ili shughuli zote za kuhudumia wananchi zifanyike kwenye Kata hiyo na hivyo kuwapunguzia umbali wa kufuata huduma.
Pia alitoa wito kwa wananchi, kulipia umeme kwa wingi kwani itasadia kuenea haraka kwa umeme nchini na hivyo kuchochea maendeleo ya wananchi.