Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( mwenye kilemba chekundu)na
Mbunge wa Bagamoyo, Shukuru Kawambwa( kulia) wakiweka jiwe la
msingi kuzindua Utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme katika vijiji
vilivyopo pembezoni mwa Miji( Peri-Urban) katika Wilaya ya Bagamoyo
mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( mwenye kilemba chekundu)na
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete ( mwenye kofia) wakikata utepe
kuzindua utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme katika vijiji vilivyopo
pembezoni mwa miji( Peri-Urban) katika Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( kulia) akiwatambulisha kwa
wananchi, Wakandarasi kampuni ya Sinotec kutoka nchini China
wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme katika Vijiji vilivyopo
pembezoni mwa Miji( Peri-Urban) katika Mkoa Pwani
Mbunge wa Bagamoyo, Shukuru Kawambwa( wa pili kushoto), Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijiji ( REA) Wakili Julius
Bundala Kalolo( tatu kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati
vijiji ( REA) Mhandisi Amos Maganga wakicheza ngoma asili ya wenyeji wa
Bagamoyo, wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme katika
Vijiji vilivyopo pembezoni mwa Miji( Peri-Urban) wilayani Bagamoyo mkoani
Pwani.
Baaadhi ya wanafunzi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu(
hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme
katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa Miji( Peri-Urban) wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani.
*************
Na Zuena Msuya, Pwani
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema ni marufuku kwa
mkandarasi yeyote kuagiza nje ya nchi vifaaa kwa ajili ya kutekeleza Mradi
wa Usambazaji Umeme katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa Miji(Peri-
Urban).
Mgalu alisema hayo kwa nyakati tofauti, Agosti 6, 2019, wakati akiweka
jiwe la msingi kuzindua Mradi wa Usambazaji Umeme katika vijiji vilivyopo
pembezoni mwa Miji(Peri-Urban) katika Kijiji cha Sanzale wilayani
Bagamoyo na katika Kijiji cha Kaloleni wilayani Chalinze Mkoani Pwani.
Katika uzinduzi huo, Mgalu alisema kuwa kwa Sasa Tanzania ina viwanda
Tisa vinavyotengeneza vifaa na miundombinu ya Umeme ikiwemo nguzo,
nyaya, Mashine za LUKU, Transfoma pamoja na vifaa vingine, hivyo
wakandarasi hao watumie vifaa vinavyotengezwa na viwanda vya ndani ili
kukuza uchumi.
Sambamba na hilo, aliwataka wakandarasi hao kufanya kazi usiku na
mchana ili kukamilisha mradi huo kwa wakati na kusitokee visingizio
vyovyote kwa kuwa vifaa vyote vinapatikana nchini.
"Wakandarasi tunatarajia mradi huo utakamilika kwa wakati, na
hakutakuwa na sababu ya kuchelewesha kwa kuwa kila kitu kinapatikana
hapa nchini",alisema Mgalu .
Mradi wa Peri-Urban katika Wilaya za Bagamoyo na Chalinze,
utaunganisha wateja zaidi ya 4000 katika kipindi cha miezi 9 ya utekelezaji,
ambao utangarimu zaidi ya shilingi bilioni 12 hadi kukamilika kwake Katika
wilaya hizo.
Mradi huo utatekelezwa katika mikoa 9 nchini kwa gharama ya zaidi ya
shilingi trilioni moja, na katika Mkoa wa Pwani pekee Mradi huo utagharibu
zaidi ya shilingi bilioni 37.
Mkandarasi anaetekeleza mradi huo katika Mkoa wa Pwani ni kampuni ya
ukandarasi ya Sinotec kutoka nchini, China.
Katika hatua nyingine Mgalu alilitaka shirika la umeme nchini Tanesco
kushughulikia kwa wakati malalamiko na changamoto mbalimbali
zinazotolewa ya wateja ili kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri baina
ya wateja na shirika hilo.
Alisema hafurahishwi na baadhi ya ujumbe au na malalamiko anayopokea
kutoka kwa wananchi wakilalamikia kutoshughulikiwa changamoto zao na
Tasesco wakati ni haki yao ya msingi kutatuliwa matatizo hayo.
Alitaka shirika hilo kuongeza kasi ama nguvu kazi katika kutatua
changamoto mbalimbali wanazozipata wateja ikiwepo kuunguza vitu
,nyumba, huduma ya umeme kwa wakati husika.