Home Mchanganyiko Bashe: Tutaweka mazingira rafiki ushiriki wa benki katika kilimo Simiyu.

Bashe: Tutaweka mazingira rafiki ushiriki wa benki katika kilimo Simiyu.

0

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, akizungumza na wafanyakazi wa NMB kwenye banda la benki hiyo wakati wa uzinduzi wa maonesho ya nanenane katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (wa pili kushoto) akitazama Bidhaa za mfanyabiashiara Raphael Buja (Buja Pure Honey) kwenye banda la NMB, wakati wa uzinduzi wa maonesho ya nanenane katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu, kushoto ni Meneja Mwandamizi Biashara na Kilimo wa NMB John Mchunda, Mkuu wa Idara ya biashara kwa Serikali kutoka NMB Vicky Bishubo (aliyevaa skafu).

*******

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kuwa wakati serikali ikijiandaa kufanya marekebisho makubwa ya sera ya kilimo, taasisi za kifedha nchini zitajumuishwa katika kutoa maoni jinsi gani zinaweza kushiriki kikamilifu kwenye kilimo.

Alisema kuwa serikali kupitia wizara ya kilimo imepanga kuweka mazingira rafiki kwa taasisi za kifedha ili ziwekeze kwenye sekta hiyo, ikiwa pamoja na kuangalia mfumo gani sahihi wa utolewaji mikopo kwa wakulima.

Naibu Waziri huyo ameyasema hayo jana wakati alipotembelea banda la Benki ya NMB kwenye maonyesho ya sikuu ya wakulima kitaifa (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Alisema kuwa kumekuwepo na tatizo la pembejeo hasa kwenye kilimo cha pamba, ambapo serikali kupitia bodi ya pamba imekuwa ikitumia fedha nyingi kuziagiza na kupelekwa kwa wakulima lakini matokeo yamekuwa hayaonekani.

“Nitakutana na taasisi zote za fedha tufanye majadiliano kwenye sera mpya wa kilimo wao wanaweza vipi kushiriki moja kwa moja mpaka kwa wakulima, wanaweza vipi kuweka mfumo mzuri na rahisi wa kutoa mikopo kwa wakulima wa chini”. Alisema Bashe.

“ Tunahitaji benki zihusike katika kubadilisha mfumo wa kuagiza pembe nje, tuache kutumia mawakala na baadala yake twende moja kwa moja viwandani kwa kutumia fedha zao na zitarejeshwa na wakulima mara baada ya kuvuna”. Aliongeza Bashe.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Biashara za serikali Vicky Bishubo kutoka NMB alisema kuwa taasisi za kifedha kujumuishwa kwenye marekebisho ya sera hiyo ni suala muhimu.

Alisema NMB kupitia kilimo biashara (Agri-business) utakuwa wakati sahihi katika kuhakikisha wakulima na wajasliamali nchini wanawezeshwa zaidi kupitia vikundi vyao ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji.

Aliongeza kuwa NMB inatambua kuwa inalo jukumu kubwa la kuhakikisha wakulima na wananchi wote maeneo ya vijini, wanajumuishwa katika mfumo rasmi wa fedha kupitia kupewa elimu na mafunzo.

Naye Meneja Mwandamizi katika mahusiano ya biashara ya kilimo kutoka NMB, John Mchunda alisema kuwa benki hiyo ilitenga kiasi cha sh. Bilioni 500 kwenye kilimo- biashara kwa muda wa miaka mitano toka mwaka 2015 kwa ajili ya kusaidia mnyororo wa thamani kwenye sekta ya kilimo na wakulima wenyewe. Na baada ya fedha hizo kuisha mwaka jana, NMB imeongeza bilioni 500 nyingine kusaidia kukuza mnyororo wa thamani (Agricultural value Chain) kwa wakulima, Wafugaji na wavuvi na biashara zao.