Home Michezo MASHABIKI WA SIMBA TAWI LA MJI MKUU JIJINI DODOMA WAMETEMBELEA HOSPITALI YA...

MASHABIKI WA SIMBA TAWI LA MJI MKUU JIJINI DODOMA WAMETEMBELEA HOSPITALI YA MKOA HUO NA KUFANYA SHUGHULI ZA USAFI

0

Mashabiki wa klabu ya Simba wakikabidhi vyakula na vinywaji katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma baada ya kutembelea hospital hiyo na kufanya usafi.

Mmoja wa mashabiki wa klabu ya Simba akitoa msaada kwa wagonjwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma kuelekea siku ya Simba Day.

Mashabiki wa klabu ya Simba wakifanya usafi katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma baada ya kutembelea hospitali hiyo hii leo

******************

KATIKA kuelekea kilele cha siku ya Simba Day, Mashabiki wa Klabu hiyo Tawi la Mji Mkuu jijini Dodoma wametembelea Hospitali ya Mkoa na kufanya usafi pamoja na kutoa msaada mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa.

Mashabiki hao waliongozwa na Uongozi wa Tawi hilo ambao wamesema wameamua kufika Hospitalini hapo ili kuwafariji wagonjwa na kuonesha jinsi gani Klabu ya Simba ipo bega kwa bega na Watanzania wa aina zote.

” Simba siyo timu tu ya mashabiki hii ni timu ya Watanzania, tumefika katika Hospitali hii ya Mkoa tumefanya usafi na kugawa msaada kwa wagonjwa, lakini pia tumetembelea kituo cha watoto yatima kilichopo Kijiji cha Matumaini na kugawa zawadi kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo,” amesema Diwani wa Buigiri, Mhe Kenneth Yindi.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Tawi hilo, Mhe Yindi ameupongeza uongozi wa Simba Makao Makuu kwa namna ambavyo wameongeza ubunifu katika Wiki ya Simba kulinganisha na miaka mingine.

Pia amechukua nafasi hiyo kupongeza usajili uliofanywa kwa ajili ya msimu ujao na kutamba kutetea taji lao la Ligi sambamba na kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa.

Nae Naibu Katibu wa Tawi hilo, Pendo Emmanuel amesema walichokifanya leo ni kuonesha jinsi gani Simba iko karibu na Watanzania na imekua ikijali watu wote walio na changamoto bila kujali itikadi za kishabiki.

” Simba ni Timu ya kila Mtanzania, sisi tunaiwakilisha Nchi Kwenye mashindano ya Afrika lazima tujumuike na Watanzania wenzetu wenye changamoto mbalimbali,” amesema Pendo.

Awali uongozi wa Simba Makao Makuu ulitoa agizo kwa viongozi wa matawi yao yote nchini kuhakikisha wanahamasisha wanachama na mashabiki wao kutembelea Hospitali na Vituo vya Afya nchini kwa ajili ya kutoa damu, kufanya usafi ba kuwafariji wagonjwa.