************
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ameagiza kuondolewa kwa Bw.
Efraz Mkama katika nafasi ya Uratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF) Mkoa wa Kagera kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi.
Dkt. Mwanjelwa ametoa maagizo hayo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa
Kagera, Prof. Faustin Kamuzora baada ya kutembelea walengwa wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Bukoba kwa lengo
la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kukutana na Watumishi wa
Umma kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri huyo, amesema utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini unapaswa kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli ambayo ina dhamira ya dhati ya kuziwezesha kaya
maskini kuboresha maisha.
Dkt. Mwanjelwa ameonyesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mratibu
huyo wa TASAF Mkoa wa Kagera na hivyo kutaka nafasi hiyo apewe
mtumishi mwingine ambaye ana vigezo na uwezo wa kutekeleza maagizo
ya Serikali kikamilifu kupitia utaratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwanjelwa ameridhishwa na mafanikio
yaliyopatikana tangu kuanza kutekelezwa kwa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini katika nyanja za elimu, afya, uzalishaji mali na ujenzi wa nyumba
unaofanywa na walengwa wa mpango huo mkoani Kagera.
“Nimejionea namna wanufaika wanavyotumia rukuzu wanayoipata
kuboresha maisha yao kwa kujenga nyumba bora za kuishi,
kujishughulisha na kilimo, ufugaji na kugharamia mahitaji muhimu ya elimu
na afya,” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Dkt. Mwanjelwa amesema, kwa kutambua mchango wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini, Serikali imeamua kutekeleza sehemu ya pili ya
Mpango huo ambayo itatilia mkazo zaidi kwa walengwa kufanya kazi katika
miradi itakayoibuliwa kwenye maeneo yao na kupata ujira kama njia
mojawapo ya kuijiongezea kipato.
Akizungumzia suala la kutotekelezwa kwa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini katika baadhi ya maeneo, Naibu Waziri huyo amesema, Serikali
imeamua kutekeleza Mpango huo katika maeneo yote nchini ili kuwafikia
wananchi wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na umaskini.
Dkt. Mwanjelwa yuko mkoani Kagera katika ziara ya kikazi kujionea
utekelezaji wa shughuli za TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi
wa Umma katika Halmashauri zote za mkoa huo.