Jaji Kiongozi Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akitoa mada kwenye kikao kazi cha wataalam kutoka taasisi mbalimbali wanaofanya Maboresho ya Mfumo wa Haki Jinai nchini ili uendane na wakati. Wataalam hao ambao ni kundi la pili wanapitia mnyororo wa haki jinai na kubainisha changamoto katika mfumo na kupendekeza hatua za namna ya kutatua changamoto hizo na hivyo kuwa na mfumo mpya wa haki jinai ambao utazingatia utoaji haki kwa wananchi.
***************
Jaji Kiongozi Dkt. Eliezer Feleshi ataka vifungo vya nje vitumike ili kupunguza msongamano magerezani.
Dkt. Feleshi ameyasema hayo alipotembelea kikosi kazi cha Maboresho ya Mfumo wa Haki Jinai kinachoendelea na maboresho hayo jijini Dodoma ambapo wataalam kutoka taasisi mbalimbali wanakutana ili kuona namna bora ya kuboresha mfumo mzima wa haki jinai ili kuwawezesha wananchi kupata haki zao.
“Makosa yote ambayo hayahitaji kifungo cha mda mrefu, maisha na kunyongwa yangepewa vifungo vya nje, huu mfumo ulianzia Uingereza karne ya 17 ambapo magereza yao yalijaa wafungwa wakapelekwa Australia na baade wakaanzisha huu mfumo. Ni vyema ukatumika ili kupunguza msongamano magerezani ”, amesema.
Vilevile aliongeza kuwa Mashauri yote mahakamani yana ukomo wa kuyasikiliza na
kuyatolea maamuzi ambapo Mahakama za chini ni mwaka mmoja na Mahakama kuu ni miaka miwili hivyo ni vyema mashauri yakaisha kwa wakati ili kuepuka mlundikano wa mahabusu magerezani.
Ameongeza, Ili kuwa na mwelekeo mzuri wa mfumo wa haki jinai, Polisi, Uhamiaji,
TAKUKURU, Idara za Wanyamapori, TRA, nawengineo ni lazima wafanye kazi kwa ukaribu na kwa kushirikiana na ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali na sio kila kimoja kufanya kazi zake bila kuwa na ushirikiano na ofisi hii muhimu na hii itaharakisha umalizaji wa mashauri Mahakamani.
Dkt. Feleshi ametembelea kikosi kazi cha wataalam wanaoshiriki katika majadiliano ya kuboresha mfumo wa haki jinai nchini na kutoa mada kuhusu kibali cha Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali kufungua na kuendesha mashtaka na Usikilizaji wa awali wa shauri kwa mahakama za chini.