Home Mchanganyiko SHILATU AHIMIZA UJENZI KWA WANANCHI KUJITOLEA

SHILATU AHIMIZA UJENZI KWA WANANCHI KUJITOLEA

0

**************

Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu amewahimiza Wananchi kushiriki ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kasi kubwa ili kuchochea maendeleo zaidi kwenye jamii zao.
Gavana Shilatu aliyasema hayo kwenye mkutano wa baina ya uongozi wa shule ya Msingi Chilindu iliyopo Kijiji cha Kichangani kata ya Mkoreha na Wazazi ambao ulikuwa na malengo ya Kujadili hali ya taaluma pamoja na uibuaji miradi ya maendeleo shuleni hapo.
Gavana Shilatu aliwasisitizia Wazazi kuhakikisha wanajitolea kuiboresha miundombinu ya shuleni ambapo waliridhia kwa  kuchangia ujenzi wa vyoo kwanza vijengwe na baadae wataelekeza nguvu kwenye ujenzi wa Madarasa na nyumba za Waalimu na kusisitiza kila Mzazi kutimiza maazimio ya pamoja.
“Ni lazima tuelewane, kile ambacho kimetoka kama azimio hapa ni wajibu kila Mtu hapa kutimiza wajibu wake kutekeleza. Kikubwa tujiletee maendeleo yetu.” Alisema Gavana Shilatu.
Gavana Shilatu pia aliwasisitizia Wazazi kukemea vikali tabia ya mimba shuleni (ambayo imepungua sana kwa sasa) pamoja na utoro shuleni ambao upo wa rejareja ili Watoto waanze na kumaliza shule ipasavyo kwani Elimu ni bure inatolewa.
Kupitia kikao hicho fedha zilianza kuchangwa na Wazazi hapo hapo ambapo uongozi wa shule ndio ulipokea michango hiyo huku Wazazi wakionyesha kufurahishwa na kitendo cha wao kushirikishwa.
“Sisi hatuna shida ya kuchangia maana fedha zinatumika kwa ajili ya maendeleo yetu, kikubwa tupeane ushirikiano kama hivi leo kwa hatua zote.” Alisikika mmoja wa Wazazi kikaoni hapo.
Kikao hicho kilihudhuliwa pia na Mtendaji Kata Mkoreha, Watendaji Vijiji, uongozi na kamati ya shuleni hapo.