Home Mchanganyiko WIZARA YA KILIMO YAJA NA MKAKATI WA TAIFA WA MIAKA 10 WA...

WIZARA YA KILIMO YAJA NA MKAKATI WA TAIFA WA MIAKA 10 WA USIMAMIZI WA MAZAO BAADA YA KUVUNWA – MHE HASUNGA

0

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akizungumza jambo kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu Hassan, kuhutubia wananchi kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima, Nane Nane, yaliyoanza tarehe 1-8 Julai 2019,  katika Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga  Mkakati wa Taifa wa miaka 10 wa Usimamizi wa Mazao baada ya Kuvunwa wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima, Nane Nane, yaliyoanza tarehe 1-8 Julai 2019,  katika Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akitoa maelezo kuhusu Tume ya Maendeleo ya Ushirika mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu Hassan wakati wa Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima, Nane Nane, yaliyoanza tarehe 1-8 Julai 2019,  katika Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu Hassan akimsikiliza kwa makini Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima, Nane Nane, yaliyoanza tarehe 1-8 Julai 2019,  katika Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akisalimiana na Bi Vumilia Zikankuba  mara baada ya kutembelea banda la Maonesho ya kilimo la Mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili-ASDP II wakati wa Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima, Nane Nane, yaliyoanza tarehe 1-8 Julai 2019,  katika Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

 

Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu

Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inakabiliwa na changamoto
mbalimbali zikiwemo, mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa
yanachangia kupungua kwa uzalishaji na tija ya mazao, uhaba wa malisho ya
mifugo na rasilimali maji, teknolojia duni za kuhifadhi mazao baada ya mavuno,
uelewa mdogo wa wadau katika kukabiliana na upotevu wa mazao na uhaba wa miundombinu
ya masoko. 

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ameyasema hayo wakati
akimkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia
Suluhu Hassan, kwa ajili ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima,
Nane Nane, yameanza leo tarehe 1-8 Julai 2019,  katika Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Mhe Hasunga amesema kuwa wakulima na wadau mbalimbali wa
kilimo watapata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali ya bidhaa za kilimo  ili kuona hali halisi ya Maadhimisho pamoja na
teknolojia za uzalishaji,  uongezaji
thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, zilivyoandaliwa. Waoneshaji
wengine wako njiani na tunatarajia uwanja huu wa Nyakabindi utafurika kwa
maonesho.

Alisema kuwa ili kuweza kukabiliana na baadhi ya
changamoto hizo za upotevu wa mazao baada ya kuvuna, Wizara ya Kilimo
imetayarisha Mkakati wa Taifa wa miaka 10 wa Usimamizi wa Mazao baada ya
Kuvunwa.

Alisema kuwa Mkakati huo umeandaliwa ili kuendana na
malengo endelevu ya dunia ya kutokomeza njaa ifikapo 2030, kuhakikisha usalama
wa chakula na lishe na kukuza kilimo endelevu kama lengo la pili la Umoja wa
Mataifa kati ya Malengo 17.

“Katika utafiti uliofanyika inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka
2050 watu watakuwa bilioni tisa (9) na hivyo mahitaji ya chakula yatakuwa asilimia
60 zaidi ya mahitaji ya sasa. Hivyo basi mkazo utakuwa kuzalisha chakula kati
ya asilimia 50 – 70 zaidi ya sasa. Hivyo, udhibiti wa upotevu wa mazao ya
chakula ni suala muhimu na la kipekee” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

Mkakati huo utakuwa Mwongozo kwa Sekta za Umma na Binafsi
katika kukabiliana na changamoto ya upotevu wa Mazao baada ya mavuno. Aidha,
Mkakati huo umezingatia mabadiliko yanayoendelea ya Kitaasisi na Kisera.

Alisema, suala la udhibiti wa upotevu wa mazao ya chakula
ni suala muhimu na la kipeee, linalopaswa kupewa kipaumbele na kila Mdau katika
mnyororo wa thamani na shabaha yetu ni kupunguza upotevu kwa asilimia 50 ya
mazao ya chakula ifikapo 2025. 

Waziri Hasunga ametaja Mkakati huo kuwa una malengo makuu
tisa ambayo ni Kujenga uelewa  kuhusu
usimamizi wa mazao baada ya kuvuna ili kuboresha ufanisi na kupunguza upotevu
wa mazao katika mnyororo wa thamani; Kuhamasisha upatikanaji, ufikiaji, unafuu
na utumiaji wa teknolojia na mbinu zilizothibitishwa kupunguza upotevu wa mazao
baada ya kuvuna; Kuwezesha mifumo ya masoko ya kilimo, ili kuboresha
upatikanaji wa soko na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna; na Kuhamasisha
tatifi na uvumbuzi wa teknolojia mpya inayoendana na mazingira yetu pamoja na
mbinu za kupunguza upotevu wa mazao.

Mikakati mingine ni Kupitia na kuweka sheria mpya ili
kuhakikisha kuwa viwango vya ubora vinazingatiwa kwa mujibu wa sheria ili
kupunguza upotevu baada ya kuvuna; Kuimarisha uwezo wa taasisi, uratibu,
ushirikiano, ubia na ushiriki wa Wadau wa usimamizi wa upotevu baada ya kuvuna
katika kuimarisha utekelezaji malengo ya kimkakati; Kutengeneza mifumo ya
usimamizi wa mazao  baada ya kuvuna ili
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi; Kukabiliana na upungufu wa
fedha katika kugharamia usimamizi wa mazao baada ya kuvuna; na Kuwa na mbinu za
kiwango kinachokubalika za kukusanya taarifa za upotevu wa mazao baada ya
kuvuna nchini.

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine
wameandaa mpango wa kutekeleza Mkakati huo. Ili kutekeleza mpango na malengo
hayo kwa ufanisi ni vema kushirikikana Wadau wote kwenye mnyororo wa thamani.