Baadhi ya kinamama wanaonyonyesha wakipita kwa maandamano maalum mbele ya mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji iliyofanyika katika kijiji cha Kisumba Wilayani Kalambo.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda akiongea mbele ya wananchi walioweza kuhudhulia katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji iliyofanyika katika kijiji cha Kisumba Wilayani Kalambo.
************
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda amewatahadharisha kinababa wenye tabia ya kunyonya maziwa ya kinamama wanaonyonyesha kwani hicho ni chakula maalum kwaajili ya mtoto aliyezaliwa na yeyote anayefanya hivyo anadhulumu haki ya mtoto ambaye hutegemea maziwa ya mama kwa muda wa miezi sita bila ya kula chakula cha aina yoyote.
Amesema kuwa kazi kubwa ya kinababa ni kuwawezesha kinamama kupata lishe bora ili wawe na afya thabiti kutoa maziwa ya kutosha na kuweza kuwanyonyesha watoto wao na kuongeza kuwa katika mkoa wa Rukwa asilimia 81 ya watoto wenye umri chini ya miezi sita wanalishwa vyakula vingine vya ziada, jambo ambalo halikubaliki kwa maendeleo ya mtoto.
“Ujumbe wa Leo ni kwamba watoto wadogo chini ya Miezi Sita ndio wanaotakiwa kunyonyeshwa, kwahiyo kinababa na wao wenye kupenda maziwa ya baba waache kwasababu hicho sio chakula chao ni lishe kwa watoto wachanga, tusidhulumu haki za watoto za unyonyeshaji, tuache tabia ya kunyonya maziwa ya mama kwa wasiohusika,” Alisisitiza.
Aidha alisema kuwa tafiti zinaonesha kuwa asilimia 17 ya watoto wenye umri chini ya miezi 6 wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa kinywaji au chakula kingine kama inavyoshauriwa na Shirika la Afya Duniani. Hii ina maana kuwa asilimia 83 ya watoto wenye umri huo hawanyonyeshwi ipasavyo.
Mh. Mtanda aliyasema hayo katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji kimkoa katika Kijiji cha Kisumba, kilichopo Wilaya ya Kalambo akimwakilisha aliyetakiwa kuwa mgeni rasmi wa uzinduzi huo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya aliisifu timu ya afya ya Mkoa kwa kuwezesha kufanyika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji katika Kijiji cha kisumba kutokana na Kijiji hicho kuwa na kinamama wengi wanaonyonyesha.
“Katika Kijiji hiki Mheshimiwa mgeni rasmi kuna Kaya 1300, na kwa takwimu ambazo tunazo kupitia idara yetu ya afya kinamama wanaonyonyesha watoto katika Kijiji hiki cha Kisumba ni 234, hivyo utaona kwamba tumekuja kuhakikisha kuwa ujumbe huu unafika kwa wadau kwa njia muafaka,” Alieleza.
Halikadhalika alisema kuwa maadhimisho hayo yankwenda sambamba na utekelezaji wa mradi wa Lishe Endelevu unaolenga kuongeza idadi ya watoto wenye umri kati ya miezi 6 – 23 kuhakikisha kwamba wanapata vyakula vyenye mchanganyiko sahihi na kusisitiza kuwa ni muhimu kinababa kushiriki katika maadhimisho hayo ili wawe msaada mkubwa kwa kinamama.
Wakati akitoa neno la Shukrani Meneja wa Mradi wa Lishe Endelevu Ali Omar alishukuru ushirikiano anaoupata kutoka serikalini na kuwasisitiza kinamama kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha afya, kulinda uhai na maisha ya mtoto.
Asilimia 67 ya watoto wa umri kuanzia miezi 6 – 23 wanapewa vyakula ambavyo havina mchanganyiko wa kutosha, yaani mlo usiokamilika, hali inayodhihirisha kuwa, taratibu duni za ulishaji watoto ni mojawapo ya sababu za utapiamlo katika Mkoa wa Rukwa.