Katibu wa Waziri Kungulu Masakala akifuatilia hoja zilizokuwa zikitolewa na
wananchi wa kijiji cha Makere wakati wa mkutano baina yake na waziri wa Madini Doto
Biteko kijijini hapo.
Waziri wa Madini Doto Biteko akimsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya Mara baada ya kuwasili katika eneo
lililozungushiwa kiwanda cha Chokaa katika kijiji cha Makere.
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Makere alipofika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika suala la
uchimbaji wa Madini ya chokaa.
**************
Waziri wa Madini, Doto Biteko ametoa mwezi mmoja kwa Halmashauri ya
Wilaya ya Kasulu, Mamlaka ya Misitu (TFS) na Ofisi za Madini mkoani
Kigoma kukaa na kuamua namna ya kuwafanya wananchi wa makere
kuendeleza shughuli zao za uchimbaji wa chokaa zilizosimamishwa tangu
mwaka 2006 na kuepuka kuwa mafarisayo kwa kuwafanya wananchi
kufurahia rasilimali ya chokaa iliyopo katika eneo lao.
Biteko ametoa kauli hiyo tarehe 30 Julai, 2019 alipokuwa katika mkutano
na wachimbaji wadogo na wananchi wa kijiji Makere kilichopo katika
halmashauri ya Kasulu Mkoani Kigoma alipofika ili kusikiliza changamoto
zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi.
Aliendelea kuwataka watumishi hao kuepuka kuwa kama mafarisayo kama
walivyotajwa katika Biblia na kubainisha kuwa mafariisayo walikuwa
wakiwabebesha wengine mizigo mizito ambayo wao wenyewe
hawakuweza kuibeba.
Biteko alizitaka mamlakahizo kuhakikisha kuwa zinaupitia mpango wa
uchimbaji Usioadhiri Mazingira (EPP) uliwasilishwa serikalini na kuonesha
kuwa na mapungufu na kurekebisha mapungufu hayo.
Aliendelea kusema, ni wajibu wa watumishi wa hao wa Halmashauri,
madini pamoja na Mamlaka ya Misitu kuhakikisha wanarekebisha kasoro
hizo ili wananchi haowaweze kuendelea na shughuli za uzalishaji na
wachangie maendeleo yao na ya Taifa kupitia kodi watakazokuwa
wakilipa.
“Wajibu wa kuwasaidia wananchi hawa ni wenu, hata mkisema
hawaruhusiwai kuchimba mje na maelezo yanayojitosheleza na
kuwaelekeza wananchi kwani wajibu wa kuwaelimisha ni wenu” alisisitiza.
Biteko alieleza mamlaka hizo kuwa kila mahali pana rasilimali ambazo
mwenyezi Mungu ameziruhusu kuwepo ili kuwasaidia katika kuendesha
maisha yao na mji wa Makere Mungu aliweka chokaa hivyo ni vyema
wananchi wakatafutiwa namna bora ya kufanya uchimbaji huo bila ya
kuathiri mazingira na si kuwasimamisha.
“Kama ilivyo dhahabu Geita, Almasi Shinyanga, Tanzanite Mirerani, asali
Tabora, na utajiri mwingine mwingi kama unavyopatikana katika maeneo
mengine, wananchi wa Makere nao wamepewa chokaa, sasa tuwasaidie ili
watumie rasilimali hiyo kuboresha maisha yao” Biteko alisisitiza.
Wananchi hawa walianza uchimbaji toka mwaka 1978 mpaka uchimbaji
huo ulivyositishwa mnamo mwaka 2006 wako katika sintofahamu,
tutawapeleka wapi wananchi hawa? Biteko alihoji.
Aidha, aliwataka watumishi hao wa umma kuja na njia mbadala kwa ajili ya
shughuli za uchimbaji wa chokaa na si kuwazuia wananchi kwa kutumia
sababu ya kukosa nishati mbadala kwa ajili ya kuchomea chokaa hiyo
isipokuwa wao wawasilishe mapendekeo yatakayowawezesha wananchi
kuondokana na adha hiyo.
“Hakuna sheria inayozuia watu kuchimba, sheria inatoa utaratibu wa
namna gani bora ya kuchimba, wapeni huo utaratibu waufuate ili waweze
kuchimba na kubadilisha maisha yao, hiyo ndio rasilimali waliyopewa watu
wa Makere, waacheni wachimbe” alisisitiza.
Kwa upande wake Meneja Misitu wa Wilaya ya Makere, Donald Kabigi
alisema walikwisha kuwapa maelekezo wananchi hao ya kufuata ikiwa ni
pamoja na kutoa matanuru ya kuchomea chokaa hiyo nje ya hifadhi yam
situ wa Makere ili kuwawezesha wataalamu kusimamia shughuli hizo
jambo ambalo bado hawajalifanyia kazi.
Akizungumzia suala la Mpango wa Hifadhi ya Mazingira (EPP) Donald
alikiri kuwa ulikuwa na mapungufu na kukiri kuwa wamepewa mwezi
mmoja ili kuweza kurekebisha mapungufu hayo yanayotokana na
changamoto za uchimbaji.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Saimon Anange kwa upande wake
alikiri kuwa kuna changamoto kwa watumishi wa serikali katika kulitafutia
ufumbuzi suala hilo na kumuhakikishia Waziri Biteko kuwa atalisimamia na
kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanakuja na majibu ya namna ya
kuwasaidia wananchi hao kama walivyoelekezwa.
Aidha, Kanali Anange, alimshukuru Waziri Biteko kwa kuchukua hatua ya
kufika katika Wilaya yake na kusaidia katika kutatua changamoto
zinazowakabili wananchi wake.
Baadaye Biteko aliwatembelea wamiliki wa kiwanda cha chokaa cha
Makere (MAKERE LIME) na kufurahishwa kwa namna wanavyofanya kazi
zao ambapo wanathaminisha madini hayo na kuyaweka tayari kwa
kuuzwa.
Biteko alilitaka kampuni hilo kujitangaza kupitia maonesho mbalimbali ili
madini hayo yaweze kuuzwa nje ya Kigoma na kuwaletea faida kubwa
jambo lililopokelewa kwa bashasha na wamiliki wa kiwanda hicho.