Eneo la Gati linaloendelea kujengwa katika Bandari ya Kabwe iliyopo Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo (wa tatu toka kulia) alipotembelea ujenzi wa bandari ya Kabwe, Wilayani Nkasi.
……………
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa wito kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhusu kuharakisha ukarabati wa meli ya MV Liemba ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na wananchi wanaoishi katika mwambao wa Ziwa Tanzganyika.
Mh. Wangabo amesema kuwa wananchi hao wamekuwa wakiweka maisha yao hatarini kwa kutumia vyombo kama mitumbwi na boti ambavyo usalama wake ni mdogo ukilinganisha na meli kubwa ya MV Liemba ambayo usalama wake ni wa uhakika.
“Nitoe wito kwa wizara husika hii meli ya MV Liemba nimeambiwa hapa kwamba ikipita kwenda Zambia inaitwa ‘Our Baby’ mtoto wetu, sasa huyu mtoto wetu anaulizwa yuko wapi, Zambia wanauliza, sasa Wizara husika twende haraka isimamie hili jambo, MV Liemba itengenezwe, watu maisha yao yapo kwenye hatari kubwa ndani ya hili ziwa Tanganyika”
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipotembelea mradi wa usanifu na ujenzi wa bandari ya Kabwe iliyopo kata ya Kabwe katika Wilaya ya Nkasi ili kujionea maendeleo ya ujenzi huo ulioanza tarehe 1 Aprili,2018 ambapo hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 52 katika miezi 14 na unatarajiwa kukamilika tarehe 1 Aprili 2020 na kugharimu Shilingi Bilioni 7.49 ambazo ni fedha za Mamlaka ya Bandari nchini.
Naye Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini Mh Ali Kessy alieleza kuwa meli hiyo ya MV Liemba ilitakiwa kukamilishwa ukarabati wake tangu mwaka wa fedha 2017/2018 lakini fedha za ukarabati hazikutengwa na kudai kuwa Waziri wa Fedha Mh. Filipo Mpango amemuhakikishia kuwa fedha za ukarabati wa meli hiyo zimetengwa katika bajeti yam waka 2018/2019.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Pasivo Ntetema amesema kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa gati, jengo la kupumzikia abiria, jengo la mgahawa, ofisi, ghala la kuhifadhia mizigo, nyumba za wafanyakazi na uzio na kuongeza kuwa kwa Bandari ya Kabwe peke yake wastani wa usafirishaji kwa mwezi ni tani 1500 hadi 2000 na mwaka wa fedha 2018/2019 zimesafirishwa tani 20,000
“Pamoja na changamoto za miundombinu lakini utaona kuna ‘access’ nzuri ya watu kupita hapa kwahiyo kukishaboreshwa bandari hii ikakamilika lakini pia miundombinu ya barabara ya kuingia hapa ikakamilika ni Imani yetu watu wa bandari ya kwamba kupitia uongozi wako, kupitia mheshimiwa mbunge na mamlaka zote zinazotawala mkoa wa Rukwa pamoja na serikali kuu, tutaangalia sasa uwezekano wa kuboresha barabara hii kwa kiwango cha lami ili shehena kubwa iweze kupita hapa
Mamlaka ya Bandari inatekeleza miradi mitatu katika Mkoa wa Rukwa ambayo ni Mradi wa uboreshwaji wa bandari ya Kasanga iliyopo Wilaya ya Kalambo, Ujenzi wa barabara katika Bandari ya Kipili na Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Gati Bandari ya Kabwe zilizopo katika Wilaya ya Nkasi ambapo miradi yote itagharimu shilingi bilioni 12.7