*******
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema amekuwa na ndoto ya muda mrefu ya kuona shule ya sekondari Liuguru inabadilishwa na kuwa shule ya bweni kwa ajili ya wasichana pekee.
“Ndoto yangu ni kuona shule hii inakuwa ya wasichana peke yao. Na tukifanikiwa, tutatengeneza akinamama wasomi, wanaojitambua, wenye maadili mema na wachapakazi,” alisema.
Alikuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Liuguru, kata ya Narungombe, wilayani Ruangwa jana jioni (Jumatatu, Julai 29, 2019) mara baada ya kukagua shule hiyo.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, alisema amechagua shule za Mnacho na Liuguru ziwe ni za bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike tu kama njia ya kuwaongezea fursa za masomo katika wilaya hiyo.
“Leo nimekuja kuwaeleza ndoto yangu. Tunahitaji kuona kila mtoto anayeenda shule, anakuwa na uhakika wa kumaliza masomo yake ya elimu ya juu. Wilaya hii tuna shida ya idadi kubwa ya mimba kwa watoto wa kike, na mimi hili jambo linanikera sana,” alisema.
“Tulikubaliana tuwe na kaulimbiu yetu kwamba ‘Ruangwa kwa maendeleo inawezekana’, lakini kwenye elimu tumekwama kuleta maendeleo kwa sababu dada zetu hawamalizi shule na sisi ndiyo wasababishaji. Tumeweka sheria ya kuwafunga watu wanaowapa mimba wanafunzi, lakini bado haisaidii.”
“Njia pekee ya kuondokana na tatizo hili ni kufanya shule hizi ziwe za bweni ili wakae hapa shuleni, wafundishwe bila kupoteza muda wa kwenda nyumbani au kukutana na vikwazo wawapo njiani kuja shule au kurejea nyumbani,” alisema.
“Kwa wenzetu kwenye mikoa mingine, mtoto wa kike akianza shule ya awali, atamaliza ya msingi, ataenda sekondari hadi chuo kikuu. Akimaliza kusoma, anarudi nyumbani kuja kufanya kazi kwao na kuwasaidia wengine waliokosa fursa.”
“Tunahitaji mabweni kwa ajili ya watoto wetu wa kike kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, tunahitaji nyumba za walimu ili wake hapa na kuwalea wanafunzi wetu. Yakikamilika, tutawahamisha wavulana wanaosoma hapa na kuwapeleka shule za jirani au za bweni, ili hapa tuwaachie wasichana peke yao,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema kwa kuanzia zitatumwa sh. milioni 100 ili zitumike kujenga nyumba nne za walimu, kisha atatafuta fedha nyingine ajili ya ujenzi wa mabweni, bwalo la chakula, jiko na mahitaji mengine kadri fedha zitakavyopatikana.
Aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wahakikishe wanakazania masomo kwani hakuna muujiza wa kufaulu mitihani kama hawatasoma kwa bidii. “Wanangu wa Form 2 na Form 4 hakuna muujiza wa kufaulu mitihani iliyo mbele yenu. Ni lazima msome kwa bidii. Na msikubali kuishia Form 4, lazima mwende Form 6 na mkimaliza hakikisheni mnafika chuo kikuu,” alisisitiza.
Mapema, akiwasilisha taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Samuel Diwani alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007, hivi sasa ina walimu 11 ambapo watatu kati yao wanafundisha masomo ya sayansi na wanane waliobakia wanafundisha masomo ya lugha na sanaa.
Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 109 ambapo 51 kati yao ni wavulana na 59 ni wasichana, inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa nyumba tisa za walimu, ukosefu wa maabara mbili na iliyopo moja haijakamilika kwa asilimia 100.
Nyingine ni ukosefu wa mabweni, maabara ya kompyuta, mfumo wa umemejua, maktaba, jengo la utawala na stoo.