Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akinyanyua bango lenye ujumbe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo ya masoko na zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa waataalam wa Maendeleo ya Jamii leo Jijini Dodoma kushoto kwake ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasha pikipiki wakati zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa waataalam wa maendeleo ya Jamii leo Jijini Dodoma.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua moja ya banda la Mwanamke mjasiliamali kabla ya kufanya uzinduzi wa Mradi wa Kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo ya masoko Nchini leo mjini Dodoma.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kwa ajili kukabidhi pikipiki wakati zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa waataalam wa Maendeleo ya Jamii leo Jijini Dodoma wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binith Mahenge, wa pili kutoka kulia ni Waziri wa Afya Bi Ummy Mwalimu na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la UN Women Bi. Ahodan Addou na viongozi wengine.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba yake wakati uzinduzi wa Mradi wa Kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo ya masoko na zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa waataalam wa Maendeleo ya Jamii leo Jijini Dodoma.
*************
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema watu wanatumia matusi ni watu waliokosa malezi kwa namna tofauti tangu wakiwa wadogo hivyo kuitaka Jamii ya Watanzania kutumia nguvu nyingi katika malezi ya watoto ili kuepukana na athari za ukosefu wa malezi ukubwani.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo jijini Dodoma katika hotuba yake ya uzinduzi wa Mradi wa Kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo ya masoko na zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa waataalam wa maendeleo ya Jamii leo Jijini Dodoma.
Aidha Makamu wa Rais amekemea wanaume wanaotumia lugha ya matumisi katika maeneo ya masoko kuwa yanasabababisha wakina mama wafanya biashara Sokoni kukosa uhuru na hata kushindwa kuleta watoto wao sokoni kwa ajili ya kuwasaidia kwa kutopenda vijana wao kusikia lugha isiyokuwa na maadili.
“Mnawazalilisha wanawake kwa kuwatukana matusi kwa kutumia viungo vyao, kuwashika au kuwapapasa bila idhini yao kwanini nyie wanaume msishikane wenyewe vitendo vya kuwazalilisha wanawake havikubaliki kabisa’’. Alisisitiza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hotuba yake hiyo Makamu wa Rais wa Tanzania amesema vitendo hivyo vya ukatili havikubaliki na ndio maana ya ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ibala ya 168 c inasema wanawake wanayo haki ya kulindwa dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote ile hivyo hatua za kukomesha vitendo vya ukatili dhidi yao ni utekelezaji wa ilani hiyo.
Pamoja na kukemea vitendo hivyo Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wanaume wanaonyanyaswa Kijinsia wasione aibu bali watoe taarifa kwenye dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi ili iweze kufanyia kazi chanagamoto hiyo.
Aidha Makamu wa Rais amehoji wanawake walio katika Kamati ya Soko kwanini wanafumbia macho vitendo vya ukatili ili hali wao ni viongozi watoa maamuzi sokoni hapo na kuonya kuwa uenda na wao wanachangia kuendelea kuwepo kwa ukatili katika maeneo ya sokoni.
Makamu wa Rais amewataka viongozi wa masoko nchini kuhakikisha wanafanyia kazi tabia ya watoto wadogo kufanya biashara sokoni kwa lengo la kusaidia familia na kuutaka uongozi wa soko kuwahoji na kuwarudisha shuleni ili kusaidia kukata mnyororo wa umasikini wa familia kwani mtoto akipata elimu inamsaidia kutumia elimu yake kupambana na umasikini.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, MAendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemwomba Makamu wa Rais kuagiza Halmashauri zote nchini kuacha kutoa kiwango kidogo cha mikopo kwa akina na mama na waongeze kiwango cha fedha ili wakinamama wapate miradi ya maana ya biashara kupitia makato ya 4% ya mapato ya kwa Halmashauri.
“Unakuta kikundi cha akina mama watano wapewa mkopo wa laki tano nakugawana fedha kidogo hii ni pesa gani ndio maana wakina mama wanaishia kuila na kushindwa kufanya marejesho kwa kuwa fedha hii inakuwa haitoshi kufanya chochote’’ Aliongeza Waziri Mwalimu.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wataendelea kutafuta na kugawa Pikipiki kwa Mikoa mingine baada ya Mkoa wa Dodoma ili kuwawezesha Maafisa Maendeleo nchini kutoa elimu kwa jamii kuhusu vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Dkt. Jingu amesema kuwa Wizara imetoa pikipiki 25 kwa mkoa wa Dodoma na mapema mwezi ujao itatoa pikipiki kumi na tano kama hizo kwa Mkoa wa Rukwa ili kuwawezesha Maafisa Maendeleo Mkoani humo kutumia usafiri huo kuelimisha wananchi kuhusu ukatili na unyanyasaji dhidi ya Wanawake na Watoto.
Naye Beatrice Siame ambaye ni Mwakilishi wanawake Soko la Majengo ameiomba Serikali kusimamia usawa wa kijinsia katika maeneo ya kazi ili wanawake waweze kunufaika na kuwezeshwa kiuchumi lakini pia akibainisha kuwa changamoto ya soko ya bidhaa zao ni kikwazo katika kumwendeleza mwanamke kiuchumi.
Uzinduzi wa Mradi wa kupinga unyanyasaji na udhalilishaji wanawake kijinsia katika Masoko ni hatua muhimu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutomeza Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto unaolenga kutokomeza vitendo vya ukatili Nchini kwa 50% ifikapo 2022.