*********
Mahakama ya Rufani leo tarehe 30 Julai,2019 imeketi kusikiliza rufaa iliyokatwa na Serikali, kupinga kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, iliyobatilisha kifungu cha 7(1) na 7(3) cha Sheria ya Uchaguzi kama ilivyorekebishwa mwaka 2015 vinayowapa Mamlaka Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji kusimamia Uchaguzi Mkuu.
Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2018 ilifunguliwa na Bwana Bob Chacha Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mkurugenzi wa Uchaguzi. Kesi hiyo iliamuliwa tarehe 10 Mei, 2019 na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Upande wa Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikuridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu ndipo walipoamua kukata rufaa.
Jopo la upande wa Serikali ambalo lilikuwa na Mawakili waandamizi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kesi hii liliongozwa na Dkt. Clement Julius Mashamba,Wakili Mkuu wa Serikali.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mahakama ya Rufani imepanga tarehe ya kutoa uamuzi.