Shule za Awali, Msingi na Sekondari za Atlas zinazomilikiwa na ‘Atlas Marc Group’ zimedhamiria kuja kivingine ili sio tu kupata matokeo mazuri zaidi bali pia kuwajenga wanafunzi wanaomaliza katika shule hizo kupata misingi mizuri itakayowasaidia maishani.
Kwa kuanzia katika harakati hizo za kufanya maboresho Shule za Atlas zilizopo Jijini Dar es Salaam katika maeneo mawili ambayo ni kampasi ya Ubungo na Madale zimeanza na mikakati kabambe katika shule zake zote.
Mkuu wa kitengo cha shule za awali katika kampasi ya Madale, Sarah Namkwahe anasema kuwa katika muhula huu wametambulisha zoezi la kujenga kujiamini miongoni mwa wanafunzi hao wa awali.
Anasema licha ya kumjenga mtoto katika kuboresha matumizi ya lugha zote mbili za kiingereza na kiswahili lakini pia kujieleza mbele ya wenzake darasani kunamjenga mwanafunzi kujiamini wakiwa mdogo.
“Hii itawafanya kuwa wanafunzi bora hata katika masomo yao ya mbele lakini vile vile kuwa watu wenye mafanikio maishani” anasema Mkuu wa kitengo cha awali.
Vile vile wametambulisha zoezi la kusoma mashairi na kuhadithia hadithi mbali mbali ili kuwafanya watoto kuwa na uelewa wa mambo mbali mbali na kujifunza pia.
Shule ya awali inayo jumla ya watoto 245 ambapo wa kiume ni 132 na kike ni 113 ambao madarasa yao yamegawanyika katika mikondo sita ikiwemo chekechea ya wadogo kabisa, (baby class), darasa la chini, madarasa mawili ya kati kati na darasa la juu la A na juu zaidi.
Mwalimu wa shule ya Msingi hapo Madale, Sarah Nalubega anasema katika shule za msingi mikakati waliyonayo ni kufundisha kwa bidii kupitia walimu wao waliobobea, pia kumekuwa na mazoezi ya mara kwa mara hasa kwa madarasa ya juu ya la sita na saba ambao wanatarajia kufanya mitihani yao mwezi Septemba mwaka huu.
Hata hivyo amesema wamekuwa na utaratibu wa kuwapa wanafunzi moyo na ushauri nasaha pale wanapokuwa na changamoto mbali mbali za kimaisha kwa vile kila mmoja anatokea katika maeneo tofauti ili kuwafanya kuwa kitu kimoja na kujiona wanaweza kufanya vizuri katika masomo yao.