Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akielezea maendeleo mbalimbali yaliyofanyika kwenye mkoa huo katika awamu hii ya tano ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli.
………………………………….
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti amesema mkoa huo unazidi kupiga hatua kwenye sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu na asiyeona maendeleo hayo atakuwa ana matatizo kichwani mwake.
Mnyeti akizungumza mjini Babati kwenye kongamano la wadau wa biashara alisema Manyara ya sasa ni tofauti na ya zamani katika suala zima la maendeleo.
Alisema miaka iliyopita mkoa huo ulikuwa nyuma kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo lakini hivi sasa inashindana na kuishinda mikoa iliyoanzishwa miaka mingi iliyopita.
Alisema mkoa huo ni watatu kwa ukubwa hapa nchini hivyo unahitaji viogozi makini na madhubuti wa kusimamia maendeleo na ndivyo wanavyofanya.
“Kwenye elimu tulikuwa nyuma lakini sasa tupo vizuri kwenye elimu ya msingi tulikuwa nyima lakini mwaka uliopita tumekuwa wanane kitaifa, kidato cha nne tulikiwa wa mwisho mwisho lakini sasa wa 12 na kidato cha sita tumekuwa watano kitaifa tunazidi kusonga mbele, alisema.
Alisema kwenye suala la miundombinu ya barabara za mkoa huo wakala wa barabara nchini (Tanroads) na wakala wa barabarab za mijini na vijijini (Tarura) wamejitahidi ipasavyo kuhakikisha inapitika kwa nyakati zote.
“Ukiacha majiji ya Dar es salaam, Mwanza na Arusha hivi sasa Babati inafuatia kwa barabara nzuri na zilizowekewa taa hadi wamasai na wairaq wanapiga picha usiku kwenye taa za kuongozea barabara tumewashinda Mbeya, Singida na Moshi,” alisema Mnyeti.
Alisema hivi sasa mkoa huo unazidi kupiga hatua kutokana na wananchi wake kuwa na fikra chanya na kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kufanya kazi na pia viogozi kuwasimamia ipasavyo.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula alimshukuru Mnyeti kwa kutangaza kuwa yeye ndiye mkuu wa wilaya namba moja ambaye ni mchapakazi na mahiri katika mkoa huo.
“Nawaahidi wananchi wa Simanjiro kuwa nitaendelea kuwatumikia bila kuchoka usiku na mchana na nawashukuru wasaidizi wangu wa karibu katibu tawala wa wilaya Zuwena Omary na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Yefred Myenzi kwani tunafanya kazi kwa ushirikiano,” alisema Chaula.