Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza
katika mkutano wa hadhara na wananchi Wilayani Malinyi,
Mkoani Morogoro, leo. Lugola amemuondoa madarakani Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha (RTO), na
kamwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara yake, kumchukulia hatua
za kisheria kwa kutokufuata maagizo anayoyatoa Waziri huyo
na kuyaita ni yakisiasa. Picha na Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akiikagua
pikipiki katika Kituo cha Polisi Malinyi, Mkoani Morogoro, leo,
ambayo imepata ajali na kusababisha dereva wa pikipiki hiyo
kufariki dunia. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura
Kasike, na Kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Polisi, ASP Evaristi
Makalla. Majura kasika Picha na Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akimpa
maelekezo Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Malinyi, Mkoani
Morogoro, SSP Ramadhan Fusi (kulia), wakati alipofanya ziara
Wilayani humo, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi.
*************
Na Felix Mwagara, MOHA-Malinyi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemuondoa
madarakani Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa
Arusha (RTO), Charles Bukombe kwa kosa la kuyapuuza
maagizo yake na kuyaita ya kisiasa.
Licha ya kumuondoa katika nafasi hiyo, Waziri Lugola
amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake, kumchukulia hatua
kali za kinidhamu RTO huyo ili iwe fundisho kwa matrafiki hao
wa mikoa nchini.
Lugola amesema RTO huyo ameshuhudia katika video ambayo
ilikua inasambaa mitandaoni akiwa katika mkutano jijini
Arusha, akipinga maagizo yake na kuyaita ya kisiasa na pia
kutokuyatekeleza.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa Mji
wa Malinyi, Mkoani Morogoro, leo, Lugola amesema yeye hatoi
maagizo ya kisiasa bali anatoa maagizo yatakayomsaidia rais
kazi zake kwa wananchi wanyonge wanaopambana na
umaskini na ajira.
“namuagiza katibu Mkuu achukue hatua za kinidhamu ikiwa ni
pamoja na kumuondoa u-RTO afanye shughuli zingine za
kipolisi, na maRTO ambao mkono wangu haujafika kwenu, na
wengine nimeanza kuwaona hamsimamii vizuri maagizo yangu,
wapo ambao wanaendelea na uonevu, wapo baadhi ya askari
wanaendelea kuchukua rushwa barabarani,” alisema Lugola.
Pia Waziri Lugola ametoa onyo kali kwa MaRTO Mikoa ya
Morogoro na Mara akiwataka wachukue fursa ya kujitathimini
katika utendaji wao kabla hajawachukulia hatua.
“Wapo baadhi ya askari waonevu, wanaendelea kuchukua
rushwa, wajitathimini, katika utendaji wao kabla sijawachukulia
hatua kali za kinidhamu,” alisema Lugola.
Lugola katika hotuba zake katika mikutano yake mbalimbali
alisema Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na haitaki
kumnyanyasa mwananchi yeyote kupitia makosa ya trafiki
wasiokuwa waaminifu.
Lugola alitoa maagizo kwa Jeshi la Polisi nchini, kuwa
bodaboda zinazotakiwa kuwepo kituo cha polisi ni zile zilizopo
katika makundi matatu ambayo ni Bodaboda zilizohusika
kwenye uhalifu, zilizotelekezwa au zilizookotwa na zilizohusika
katika ajali.
“Bodaboida hizo ndizo zinapaswa kuwepo vituoni, lakini
kuziweka bodaboda ambazo hazipo katika makundi hayo,
napiga marufuku na hii nataka Polisi nchi nzima munielewe,”
alisema Lugola.
Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda mjini Malinyi na
Tanzania kwa ujumla wafuate sheria za usalama barabarani
zikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya
mmoja na pia wakiendesha wanapaswa kuwasha taa.
Pia Waziri Lugola amepiga marufuku tabia ya baadhi ya askari
Polisi hapa nchini kukamata pikipiki wakiwa hawana sare za
Jeshi, anasema kwa kufanya hilo kunaleta kero kwa madereva
na pia anayekamatwa anaweza akadhaniwa kuwa ni jambazi.
Lugola anaendelea na ziara yake mkoani Morogoro, na
anatarajia kumaliza ziara hiyo Wilaya ya Ulanga Mkoa humo
Julai 29, 2019.