Home Mchanganyiko Asasi za kiraia na Mashirika ya Kimataifa Yatakiwa kujenga Miundombinu ya Elimu

Asasi za kiraia na Mashirika ya Kimataifa Yatakiwa kujenga Miundombinu ya Elimu

0

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu bwana Tixon Nzunda (aliyevaa suti) akizungumza mara baada ya kukagua mojawapo ya madarasa manne ya elimu ya  awali kati ya madarasa 30 yanayojengwa na asasi ya kiraia ya TAHEA chini ya ufadhili wa shirika la kimataifa kutoka nchini Scotland la Children in Cross fire wilayani Misungwi jana.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu bwana Tixon Nzunda akizungumza na wanafunzi wa elimu ya awali wa shule ya Msingi Mamae iliyopo wilayani Misungwi mara baada ya Naibu Waziri kutembelea shule za msingi Magaka na Mamae ambazo ujenzi wake ulifadhiliwa na asasi ya TAHEA wakishirikiana na shirika la kimataifa la Children in Crossfire jana wilayani Misungwi.

………………………

Na Mathew Kwembe, Mwanza

Serikali imezitaka asasi za kiraia, taasisi za umma pamoja na mashirika ya kimataifa ambayo yanafanya kazi na serikali kwenye sekta ya elimu kuhakikisha kuwa yanaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kujenga miundombinu ya elimu nchini kwa sababu ndiyo changamoto kubwa inayoikabili sekta hiyo hivi sasa.

Wito huo umetolewa jana katika kijiji cha Magaka wilayani Misungwi na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu bwana Tixon Nzunda wakati akikagua mojawapo ya madarasa manne ya elimu ya  awali kati ya madarasa 30 yanayojengwa na asasi ya kiraia ya TAHEA chini ya ufadhili wa shirika la kimataifa kutoka nchini Scotland la Children in Cross fire katika wilaya za Misungwi na Ukerewe mkoani Mwanza.

Amesema kuanzia sasa asasi zote za kiraia na mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na masuala ya elimu mbali na kufanya kazi ya kufundisha na kujenga uwezo yatalazimika kujenga angalau darasa moja pamoja na matundu ya vyoo ili kuwezesha uwepo wa mazingira rafiki ya ufundishaji na ujifunzaji kwa ajili ya watoto wanaosoma elimu ya awali nchini.

“Hatutakubali taasisi yoyote inayotaka kujihusisha na masuala ya elimu nchini kutumia raslimali kubwa katika maeneo ya  aina moja tu ya kujenga uwezo na kwenye masuala ya advocacy (ushawishi) na kuaacha kwenda kwenye matatizo ya kweli ambayo yanawakabili watoto, hasa haya maeneo ya watoto wa shule za awali,” amesema Naibu Katibu Mkuu na kuongeza:

“Kwasababu eneo hili bado hatujawekeza vya kutosha, kwa hiyo tunawataka wadau wote waje kutusaidia pale kwenye miradi mbalimbali inayohusiana na elimu ya awali kwa kutujengea angalau darasa moja kwa ajili ya choo na elimu ya awali.”

 Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa serikali sasa imeazimia kuhakikisha kuwa watoto wote walio ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanapata fursa ya kupata elimu ya awali, elimu ya msingi, na elimu ya sekondari bila ya vikwazo vyovyote.

Pia bwana Nzunda amewataka jamii na wazazi waendelee kuchangia elimu hasa katika maeneo ya chakula cha watoto wao wanapokuwa shuleni kama wanavyowajibika kuwapatia chakula watoto wao wanapokuwa majumbani kwao.

“Lengo ni kuwawezesha watoto wetu wawapo shuleni angalau wapate uji na chakula cha mchana ili waweze kusoma vizuri na kuchangamka wawapo madarasani,” amesema.

Sambamba na hilo, jambo la pili ambalo Naibu katibu Mkuu amelisisitiza ni kuwataka jamii na wazazi kuisadia serikali kwenye miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo kwa kuanza kujenga maboma kwa ajili ya watoto wanaosoma kwenye elimu ya awali,

Ameongeza kuwa kukamilika kwa maboma hayo kutawawezesha watoto wa elimu ya awali kuchangamka, wanajifunza mbinu za maisha, wanajenga mbinu za namna ya kuhusiana, wanajenga misingi ya utu, upendo, na furaha miongoni mwa watoto.

“Kwa kufanya hivi ninaamini tunaenda kujenga taifa la watoto wanaojitambua ambao wamejengewa misingi mizuri, tofauti na hao tutakuwa tunapoteza nchi na taifa,” amesisitiza Naibu Katibu Mkuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Children in Crossfire bwana Craig Ferla alimweleza Naibu Katibu Mkuu kuwa taasisi hiyo kwa kushirikiana na asasi ya kiraia ya TAHEA watajenga madarasa 100 ya aina hiyo katika mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dodoma katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Pia ameelezea kufurahishwa kwake kwa jinsi uongozi wa juu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, mkoa wa Mwanza, halmashauri ya wilaya ya Misungwi, na kata za Mamae na Magaka kwa jinsi walivyompa ushirikiano katika kufanikisha ujenzi wa madarasa hayo changamshi ya elimu ya awali katika wilaya ya Misungwi.

Bwana Craig amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa Children in Cross fire pamoja na TAHEA wana nia njema ya  kuchangia maendeleo ya Tanzania.

“Tunaamini kwamba hawa watoto wetu ambao ndiyo wako kwenye madarasa ya awali ndiyo taifa la kesho na tunaamini kuwa kama watapata mwanzo bora, wataweza kuchangia maendeleo ya taifa letu kwa ufanisi wa hali ya juu,” amesema.