Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima akisisitiza jambo wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utoaji wa huduma katika Vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na watumishi wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utoaji wa huduma katika Vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro
……………………
Na. Angela Msimbira KILOSA.
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia afya kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Dorothy Gwajima amesikitishwa na uwajibikaji mbovu wa timu ya uendeshaji wa huduma za afya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro kwa kutokusimamia kikamilifu huduma za afya zinazotolewa katika Wilaya hiyo.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua huduma za afya zinazotolewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro hivi karibuni.
Dkt. Gwajima amebaini kuwa, watumishi wapo kwa kiwango kinachokidhi ukilinganisha na idadi ya wateja wanaotumia vituo hivyo, lakini bado wateja wamekuwa wakilalamika kuwa hawaridhiki na hali ya huduma ambapo, sababu kubwa ni kutowajibika kwa baadhi ya watoa huduma na viongozi wenye dhamana ya kusimamia huduma hizo.
Ameeleza kuwa hali ya huduma inayotolewa katika vituo hivyo vya tiba inalalamikiwa kutokana na utendaji wa mazoea unaofanywa na baadhi ya viongozi wa afya ngazi ya halmashauri wenye dhamana ya kusimamia huduma za Afya.Matokeo yake wanaishia kulalamika na hawachukui hatua na pia hawabaini nini kifanyike.
Ammevitaja vituo vilivyotembelewa kuwa ni pamoja na Kituo cha Afya Ulaya, Kituo cha Afya Kimamba na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.
“Ninawaagiza watendaji hao kuamua moja, ama kuwajibika na kusimamia kwa kufuata miongozo, kanuni na maadili ya kazi na kuleta mabadiliko mara moja ama watoke kwenye nafasi za uongozi wakaendelee na majukumu yao ya msingi ambayo ndio waliomba ajira maana uongozi nao unahitaji moyo wa kujitoa”. Anasisitiza Dkt. Gwajima.
Hata hivyo, Dkt. Gwajima amesema kamwe Serikali haitasita kuendelea na operesheni ya kuwaweka pembeni watendaji wazembe ambao, pamoja na kuwa na wasifu mzuri wa kitaaluma bado hawaleti ufumbuzi wa changamoto za msingi za uendeshaji, wanalalamika tu licha ya uwingi wa semina za uwezeshaji na maelekezo.
Amesisitiza kuwa suala la kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa mazoea ndiyo unaathiri huduma na kufanya wateja wengi kuamua kutotumia huduma za vituo hivi na kwenda kuzitafuta mbali zaidi kinyume na malengo ya Serikali kuwahudumia Wananchi karibu na makazi yao ili kuokoa gharama za fedha na muda wa kwenda mbali zaidi kutafuata huduma afya.
“Haiwezekani ikifika Ijumaa na siku za mapumziko wateja hawapati huduma na haiwezekani wimbo wa upungufu wa watumishi ukaendelea kuimbwa tu kwa mazoea bila takwimu. Takwimu za hapa halmashauri ya Kilosa katika vituo nilivyotembelea zinaonesha idadi ya wateja iko chini na hakuna tabibu kwa siku anayeona wagonjwa zaidi ya 20 na kama ni zaidi basi ujue wengine wametegea”, huko wodini nako hakuna wagonjwa wengi kiasi cha kusababisha kila mtoa huduma kuhudumia juu ya kiwango, Anasisitiza Dkt. Gwajima.
Amewaagiza watumishi wote nchini kuhakikisha wanafunga hesabu ya idadi ya wateja waliowahudumia kuanzia tarehe 1 hadi 5 ya kila mwezi ili kupata takwimu sahihi ya wagonjwa wanaopata huduma katika vituo vya afya nchini.
“Kila mtumishi sasa atafunga hesabu ya idadi ya wateja aliowahudumia kila tarehe 1 hadi 5 ya kila mwezi na hapa ndiyo tutajua tuko wengi au wachache. Utaratibu huu umeshaanza tangu Mei, 2019 na nyie Kilosa nimegundua hamjatekeleza tangu kuanza, ninawaagiza viongozi hao kuwasilisha taarifa maalumu ndani ya siku 14” Amesisitiza Gwajima.
Amewataka waliopewa dhamana ya kusimamia sekta ya afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri kuhakikisha wanawajibika na kutumika kikamilifu na kutambua kwamba, kupewa dhamana ya uongozi siyo fursa ya kupumzika bali ni kutumika hivyo, wazembe, wasiojituma, wasio wabunifu na wanaopenda mialiko ya safari tu hawana nafasi kwenye timu za kazi sasa.
Amewataka kuhakikisha ufuatiliaji na usimamizi unafayika kwa tija na haki na kila eneo linakaguliwa kwa uwazi na hatua zinachukuliwa kwa wakati siyo kulalamika na kusubiri ufumbuzi waje wakaguzi toka Wizarani ndiyo upatikane.
Vilevile, Dkt. Gwajima ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa kuona umuhimu wa kutenga fedha za mapato ya ndani shilingi milioni 487,328,613 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi wa Mama na Mtoto ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambaye, amedhamiria kufikisha huduma za tiba karibu zaidi na Wananchi kwa kujenga miundombinu ya afya.
Dkt. Gwajima amesema, kwa Halmashauri ya Kilosa kwa kipindi cha mwaka 2017/18 Serikali imepeleka Tsh milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kidodi na Tsh. Mil 400 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Zahanati ya Mikumi ikidhi kuwa Kituo cha Afya na kutoa huduma za upasuaji wa dharura.
Amewapongeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ambao, wamekuwa mstari wa mbele kuwekeza rasilimali katika kuboresha sekta ya afya na kwamba, Wizara itawatambua kwa juhudi hizo.
Aidha, ametoa angalizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wao hawawi sehemu ya kuchelewesha kasi ya kuboresha huduma za afya kupitia michakato mirefu bila sababu wakati wa kutoa maamuzi kwa kuwa, taarifa zitaibua mapungufu kwa Wataalamu wa Afya halikadhalika Viongozi wenye maamuzi ya kiutawala kwa ujumla wake.