*********
******************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe *Ndugu Emmanuel Shilatu* hajaridhishwa na ujenzi mradi wa ghala uliotumia Tsh. Milioni 40 lakini umeshindwa kukamilika na kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi mara moja juu ya ujenzi huo na namna fedha hizo zilivyotumika.
Gavana Shilatu aliyasema hayo alipotembelea ghala hilo lililopo Kijiji cha Kitama Shuleni kata ya Kitama na kusikitishwa namna ambavyo fedha nyingi zikitajwa kutumika huku mradi ukiwa haujafika ukamilifu tarajiwa kiasi kinachopelekea kijiji kukosa mapato jambo ambalo ni kero kwa Wanakijiji waliokuja kulalamika kwa Afisa Tarafa huyo.
*”Serikali imetoa fedha tangu 2012 lakini mpaka sasa mradi haujakamilika na hivyo kunapelekea mapato yanakosekana ambayo yangesaidia kuleta maendeleo kijijini na maeneo mengineyo pia. Hili halikubaliki hata kidogo, naiagiza TAKUKURU kuanza uchunguzi mara moja juu ya ujenzi huu wa ghala.”* Alisisitiza Gavana Shilatu.
Mradi huo wa ujenzi wa ghala lililopo eneo la Kitama Farmers Group kwenye kijiji cha Kitama Shuleni ulianza tangu mwaka 2012 lakini hadi Leo hii haujakamilika na hivyo kukosesha Serikali mapato.
Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Mtendaji Kijiji Kitama Shuleni, Halmashauri ya Serikali iliyokuwepo Madarakani na ya sasa pamoja na Wazee maarufu Kijijini hapo ambao wote hawakuridhishwa na matumizi ya fedha ya ujenzi wa mradi huo.