***********
NA MWAMVUA MWINYI, KIBITI
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa ,Mzee Mkongea Ali amekemea kilimo cha bangi kwani kinaharibu mazingira na kuweka rehani maisha na afya ya watumiaji ambapo asilimia kubwa ni nguvu kazi ya Taifa ambayo ni kundi la vijana.
Ameeleza,licha ya hayo serikali inaendelea kupambana na matumizi ya madawa ya kulevya ikiwemo,milungi,cocaine,heroine, bangi pamoja na kudhibiti mianya ya wauzaji wa madawa hayo ili kuokoa nguvu kazi hiyo ambayo inaangamia siku hadi siku.
Hayo aliyasema wakati mbio za mwenge wa uhuru Jaribu Mpakani, kata ya Mjawa wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Mkongea alieleza Taifa letu bado kuna matumizi ya madawa ya kulevya hivyo tushirikiane kudhibiti na kupambana na janga hilo .
“Chakusikitisha vijana hawa wanaita bangi kwa majina mengi kama vile misuba,cha Arusha,jani,ganja,msokoto,Bob Marley na Jamaica lakini ukweli unabaki pale pale bangi ni bangi tu ,vijana tubadilike tupambane na janga hili na tujiingize katika shughuli za kujenga Taifa kuchapa kazi”alisisitiza Mkongea.
Hata hivyo, Mkongea aliwaasa vijana kuacha kuvuta bangi ,kujidunga sindano za madawa ya kulevya kwakuwa wanakuwa hatarini kupata ugonjwa wa ukimwi,moyo,ini,mapafu na hatimae kifo.
Akizungumzia suala la Ukimwi, mkimbiza mwenge kitaifa huyo alisema ugonjwa huo bado ni hatari jamii ijilinde na kuwa waaminifu.
“Watanzania takriban milioni 1.4 wanaishi na VVU ,maambukizi mapya kila mwaka ni watu 81,000 tuendelee kujikinga na kuwa na tahadhari na maambukizi mapya”alibainisha .
Mkongea alieleza, mkoa wa Njombe unaoongoza kwa maambulizi nchini kwa asilimia 11.4,Iringa asilimia 11.3,Mbeya asilimia 9.3,Mwanza asilimia 7.2 na Kagera 6.5 huku kitaifa ikiwa asilimia 4.7.
Kwa upande wake ,mkuu wa wilaya ya Kibiti ,GulamKifu alisema ,mwenge wa uhuru ukiwa Kibiti utapitia miradi 13 yenye gharama ya bilioni 2.59.
Alieleza katika miradi hiyo ,mradi mmoja utafunguliwa,mmoja utazinduliwa,miradi mitatu itawekwa jiwe la msingi na mingine nane itatembelewa.
Nae mbunge wa viti maalum mkoani Pwani, ambae pia ni naibu waziri wa nishati Subira Mgalu aliwahamasisha wananchi kujitokeza katika shughuli za uwekaji jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa umeme Stigo wilayani Rufiji,itakayofanyika Julai 26 mwaka huu.
Aliwaambia wananchi hao baada ya mradi huo kukamilika maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme yatanufaika na mradi huo .