Choo cha soko la matunda kinacholalamikiwa kukosa maji na milango
************
Na Mwandishi wetu, Katavi
Wafanyabiashara wa soko la matunda katika kata ya Kawajense katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya choo cha soko hilo kukosa mlango hali ambayo inawaondolea usiri; huku choo hicho kikikosa huduma ya maji licha ya kuwekewa tanki la maji hali ambayo inaweza kusababisha kupata magonjwa ya mlipuko
Wafanyabiashara hao watoa malalamiko yao katika mkutano wa hadhara uliofanyika sokoni hapo ambapo wamesema kuwa soko hilo limegeuzwa kituo cha kushushia bidhaa na kisha kutawanywa katika masoko mengine hali inayopelekea soko hilo kuzorota
Bi. Lydia Malambika ni mmoja wa wafanyabiashara soko hilo amesema wakitaka kwenda chooni wanalazimika kubeba maji ya kuingia nayo chooni
Naye Bi. Martha Kipiya amelalamikia choo hicho kukosa milango hali inayowakosesha uhuru pindi waingiapo chooni
Aidha amelalamikia suala ushuru kutozwa mara mbili ambapo amefafanua kuwa wakishusha mikungu ya ndizi na magunia ya parachichi wanaikatia ushuru lakini pia wanapopanga bidhaa hizo mezani wanakata ushuru wa soko pia
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda; Afisa Mipango wa Manispaa hiyo bwana Leonard Kilamhama amesema wataangalia changamoto zilizopo ili kuweza kuziboresha
Amesema endapo soko hilo litazungushiwa vibanda vya maduka litawezesha kuongezeka kwa wafanyabiashara hali ambayo itawezesha soko hilo kukua
Kuhusu choo kukosa milango Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini bwana Sebastian Kapufi ameahidi kupeleka fundi kwa ajili ya kutengeneza milango hiyo
Aidha amesema atashirikiana na wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi za kata hiyo