Baada ya wanafunzi wa shule ya msingi Kambarage yenye mchanganyiko na wenye ulemavu iliyopo halmashauri ya mji wa Njombe kueleza hisia zao mbele ya naibu waziri ofisi ya rais TAMISEMI Mwita Waitara juu ya changamoto ya miundombinu isiyo rafiki kwa ndugu zao walemavu pamoja na mrundikano mkubwa wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa , Serikali imeahidi kujenga darasa maalumu na choo shuleni hapo kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa madarasa mane na kupokea taarifa ya shule yenye changamoto lukuki ikiwemo upungufu wa vyumba 15 vya madarasa na vyoo vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu pamoja na chumba cha kujisafisha watoto wakike waliopevuka waziri Waitara amesema amehuzunishwa na hali ya shule hiyo na kuahidi kuipa fedha za ujenzi wa chumba kimoja cha darasa la wenye mahitaji maalumu pamoja na choo ili kupunguza adha hiyo.
Katika hatua nyingine naibu waziri huo amewataka wananchi kutoliacha jukumu la ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa serikali na badala yake watoe michango ya hali na mali ili kufanikisha ujenzi wa vyumba vingine kwa kuwa kufanya hivyo kutaboresha mazingira ya utoaji wa elimu bora mashuleni.
Given Mhanga ambaye ni kaka mkuu pamoja na Jane Ng’umbi ni mingoni mwa wengi waliotoa hisia zao mbele ya naibu waziri ambao wanasema shule hiyo imekuwa na changamoto kubwa kimiundombinu kwa kuwa ipo katikati ya mji na inapokea wanafunzi wengi zaidi hivyo ni vyema serikali ikaitazama kwa jicho la tatu.
Katika hatua nyingine naibu waziri amekagua miradi mingine sita ya maendeleo kikiwemo kituo cha afya cha Makowo ambacho kimejengwa kwa ushirikiano wa serikali , michango ya wananchi na wafadhili na kufikia hatua nzuri jambo ambalo linamsukuma mbunge wa jimbo la Njombe mjini Edward Mwalongo kumuomba waziri kuwapa vifaa tiba na madawa mapema baada ya kumaliza ujenzi kwa kuwa kituo hicho kilicho mpakani kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi wa kata jirani za wilaya ya Ludewa na Makete.