****************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo Julai 24 amemkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo baada ya Mwenge huo kukamilisha shughuli ya uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwenye miradi zaidi ya 35 maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 123.
RC Makonda amesema katika siku tano ambazo mwenge umekimbizwa Dar es salaam umefanikiwa kutembelea, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 35 ya maendeleo kwenye wilaya zote tano.
Aidha RC Makonda amewashukuru wakimbiza mwenge wa Uhuru kitaifa kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kwa siku zote walizokuwa Dar es salaam na kuwapongeza wananchi kwa ushirikiano mkubwa walioonesha tangu siku mwenge ulipowasili.
Itakumbukwa kuwa mwenge wa Uhuru uliwasili Dar es salaam Julai 19 ukitokea mkoa wa mjini Magharibi na leo umekabidhiwa Mkoa wa Pwani tayari kwa kuendelea na shughuli ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo mkoani humo.