Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally akizungumza na Wataalam wanaoshiriki majadiliano ya kufanyia maboresho ya sekta ndogo ya haki jinai nchini unaofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally akizungumza na Wataalam wanaoshiriki majadiliano ya kufanyia maboresho ya sekta ndogo ya haki jinai nchini unaofanyika jijini Dodoma.
Washiriki wa Mkutano wa Wataalam wa majadiliano yenye lengo la kufanyia maboresho sekta ndogo ya haki jinai nchini unaofanyika jijini Dodoma wakimsikiliza Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally (hayupo pichani ) alipokuwa akizungumza nao juu ya kazi hiyo wanayoifanya.
…………………..
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally ametembelea Mkutano wa Wataalam wanaoshiriki majadiliano ya kufanyia maboresho ya sekta ndogo ya haki jinai nchini unaofanyika jijini Dodoma na kuwataka wataalamu hao kushughulikia maeneo yanayotoa mianya ya rushwa, urasimu na ubwetekaji kwa taasisi zinazohusika na mfumo wa haki jinai ili kupata mfumo sahihi unaotoa haki kwa wananchi.
Amesema kazi ya maboresho ya mfumo wa haki jinai inapaswa kushirikisha taasisi zote zinazohusika na mfumo huo ikiwa ni pamoja na sheria zinazosimamia taasisi hizo ili kuziondoa katika mazingira ya ubwetekaji, urasimu na mazingira yanayotoa mianya ya rushwa.
“Huwezi kuwa na mfumo bora na thabiti wa utoaji haki nchini kama taasisi zinazosimamia na kutoa haki nchini zitakuwa zimebweteka, zina urasimu na kuwa na sheria ambazo zinatoa mianya ya rushwa, ni jukumu lenu kuangalia taasisi husika na sheria zao, na msipofanya hivyo hamuwezi kufikia lengo la kuwa na mfumo bora na thabiti utakaotoa haki kwa watu” amesema.
Amesema ni wazi kuwa taasisi nyingi zinazohusika na mfumo wa haki jinai nchini bado zinakabiliwa na kasoro hizo na kuongeza kuwa ili kuondokana nazo ni lazima taasisi zinazohusika ziondokane na vitu hivyo.
Amesema kama vitu hivyo visipozingatiwa lengo la kupata mfumo bora na thabiti wa utoaji haki kwa wananchi haliwezi kufikiwa na hivyo kukwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kutoa haki kwa wananchi.
Amewataka Washiriki kuangalia maeneo yote ambayo yanatoa mwanya wa kufanyika kwa vitendo vya kijinai ambavyo ni vya kutengenezwa na hivyo kuwakosesha wananchi haki kwa kuwa wahusika wa taasisi hizo wana mianya hiyo.
“Muangalie maeneo yote ambayo yanawapa mianya watendaji katika taasisi husika kutengeneza vitendo vya kihalifu na kuwarushia wananchi ambao mwisho wa siku wanakuwa wamekoseshwa haki zao kutokana na kukabiliwa na vitendo hivyo vya kihalifu ambavyo ni vya kutengenezwa,” amesema.
Amesema kushamiri kwa vitendo hivyo kunafanya kuanguka kwa mfumo wa haki jinai nchini ambako pia kunamaanisha kwamba taasisi zinazohusika na mfumo huo pia zinakuwa zimefeli.
Dkt. Bashiru ametoa kauli hiyo jijini Dodoma alipotembelea mkutano wa Wataalam wanaoshiriki katika majadiliano ya kuboresha mfumo wa haki jinai jinai nchini ili iweze kuimarisha utoaji haki nchini kwa wote na kwa wakati.
Wataalam hao ambao ni kundi la pili wanapitia mnyororo wa haki jinai na kubainisha changamoto katika mfumo na kupendekeza hatua za namna ya kutatua changamoto hizo na hivyo kuwa na mfumo mpya wa haki jinai ambao utazingatia utoaji haki kwa wananchi..