Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga, akifungua semina ya mafunzo ya
kuwajengea uwezo wanawake makandarasi wa mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa
na Katavi. Mafunzo hayo yanafanyika katika Chuo cha Veta mkoani Kigoma.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma Mhandisi
Narcis Choma, akizungumza na wanawake makandarasi kuhusu kuchangamkia
fursa za kazi ya matengenezo ya barabara hasa kwa mkoa huo. Mafunzo hayo
yamejumuisha wanawake makandarasi kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa
na Katavi.
Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake kutoka Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhandisi Gladiness Kitaly,
akizungumza na wanawake makandarasi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya zaidi
ya wiki moja kwa ajili ya kuwajengea ufanisi katika kazi za ujenzi na matengenezo
ya barabara, mkoani Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga, akipokea asali kutoka mwanamke
mkandarasi Bi. Rosemary Augen, ambaye pia anajishughulisha na biashara
ndogondogo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wananawake makandarasi
yanayofanyika mkoani Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga, akiwa katika picha ya pamoja na
wanawake makandarasi kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi mara
baada ya kufungua mafunzo ya makandarasi hao ya kuwajengea uwezo, mkoani
Kigoma.
Meneja wa Kanda ya Kati ya Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), Mhandisi
David Msekeni, akifundisha namna ya taratibu za kujisajili kupitia bodi hiyo kwa
wanawake makandarasi kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi
walioshiriki semina ya kuwajengea uwezo, mkoani Kigoma.
*****************
Wito umetolewa kwa makandarasi wanawake kwenye mikoa ya Kanda za
Magharibi na Nyanda za Juu Kusini kujitokeza na kuchangamkia fursa za miradi
midogo inayojitokeza katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa
mkoani Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga, ametoa wito huo wakati akizungumza
kwenye mafunzo ya wiki mbili kwa makandarasi wanawake kutoka mikoa minne
ya Kanda ya Magharibi na Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya kuwajengea uwezo
ili kushiriki kwenye kazi za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara hapa
nchini.
“Wanawake msilale changamkieni fursa za hii miradi na msing'ang'anie tu kazi
hizi za kufyeka nyasi na kuzibua mitaro kwenye madaraja bali mjitokeza hata
kwenye kazi za ujenzi wa barabara”.Amesisitiza Mhe. Anga.
Aidha, Mkuu wa Wilaya hiyo ameongeza kuwa fursa za utekelezaji wa miradi
midogo kwenye miradi mikubwa inayo nafasi kubwa ya kuwajengea uwezo wa
kitaalam na kifedha wahandisi wanawake nchini hivyo ni wajibu wao kutumia
nafasi hiyo sasa ambapo mkoa wa Kigoma unayo fursa ya utekelezaji wa miradi
mingi ya ujenzi ambayo wakandarasi wengi wanaweza kujitokeza na kuifanya.
Mhe. Anga amesema kuwa bado makandarasi wengi wanawake mkoani Kigoma
hawajajitokeza kwa wingi kushiriki kwenye miradi ya ujenzi fursa ambayo
inawanyima kukua kimtaji na uwezo wa utekelezaji wa kazi na miradi mingi ya
ujenzi.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa Kigoma,
Mhandisi Narcis Choma, amesema kuwa kwa sasa mkoa Kigoma unatekeleza
mradi mkubwa wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 260
ambapo zipo kazi ambazo wakandarasi hao wanawake wanaweza kuzifanya.
Mhandisi Choma amesema kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
kupitia Sera ya uwezeshaji wanawake kiuchumi imeweka mkakati wa kuwasaidia
na kuwapa kipaumbele kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo
inatekelezwa chini ya Wizara hiyo.
Awali Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji Wanawake katika kazi za barabara
kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Gladiness Kitaly,
amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwapa ujuzi makandarasi hao
wanawake kujua namna ya kuomba miradi ya barabara, taratibu za kujaza
zabuni za maombi ya miradi, ufanisi wa teknolojia ya nguvu kazi katika kufanya
matengenezo ya barabara katika maeneo ambayo yanatoa kipaumbele kwa
wanawake.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yameshirikisha wahandisi wanawake kutoka katika
mikoa ya Katavi, Rukwa, Tabora na wenyeji Kigoma.