*************
Na Mwandishi Wetu
MREMBO Winfrida Brayson ameshika nafasi ya kwanza kwenye shindano la Urembo la Mitindo na Utamaduni katika mashindano ya Urembo ya Viziwi ya Kimataifa yaliyofanyika kuanzia Julai 7 hadi 15 mwaka huu mjini St.Petersburg nchini Urusi.
Katika mashindano hayo Tanzania iliwakilishwa na warembo wawili ambapo Grace Mtui alishiriki mashindano hayo ya Urembo na kushindwa kufanya vizuri.
Winfrida pamoja na ushindi huo pia alishika nafasi ya 10 kwenye mashindano hayo ya Urembo ya Kimataifa ya Viziwi (Miss Deaf International) ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na mrembo kutoka Botswana, wa pili Kenya na wa tatu Urusi.
Afisa Uhusiano wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (Kisuvita), Nasiria Nasir aliyeandamana na warembo hao nchini Urusi, alisema Jana baada ya kurejea nchini kuwa licha ya kushiriki kwa mara kwanza wamejitahidi na watajipanga zaidi mwakani.
“Tumejitahidi kwa kweli lakini changamoto kubwa ilikuwa lugha ya alama ya Kimataifa, majaji walishindwa kuelewa lugha ya alama ya Tanzania kwenye usaili,” alisema.
Aidha kituo hicho cha Kisuvita kiliishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kugharamia warembo hao na Mkuu wa msafara pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Warembo hao wanatarajia kurejea nchini Julai 24 mwaka huu.