Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Deo Ndejembi amesema vijana nchini wanapaswa kumuunga mkono Mhe Rais Dk John Magufuli kwa jinsi alivyowaamini kwenye nafasi mbalimbali za uongozi
DC Ndejembi amesema kwa miaka mingi ilikuepo dhana ya vijana kuonekana hawana uwezo wa kuongoza lakini Mhe Rais Magufuli katika Serikali yake ya awamu ya tano ameteua vijana wengi kwenye uongozi kuliko awamu nyingine zote.
Amesema kwa maendeleo ambayo Rais Magufuli ameyaleta ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne anapaswa kuungwa mkono na vijana na siyo kulalamika pembeni.
Ndejembi ambaye pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho kupitia Umoja wa Vijana pamoja na Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi amewataka vijana kumuunga mkono Rais Magufuli na kumsaidia kwenye utendaji wake wa kazi katika kuwatumikia wananchi.
” Mhe Magufuli ndiye Rais wetu na ndiye Mwenyekiti wetu ndani ya Chama, mapinduzi ambayo ameyafanya kwenye Nchi hii yanapaswa kupongezwa kwa kiwango kikubwa sana.
” Leo hii chini ya Rais Magufuli Tanzania imepiga hatua kwenye sekta ya usafirishaji, tunajenga reli ya kisasa kiwango cha Kimataifa (SGR), usafiri wa anga ulikua umekufa lakini tunavyozungumza Ndege zinapishana angani kutua viwanja vya Afrika Kusini na India. Ni lazima tumuunge mkono Jemedari wetu huyu,” Amesema DC Ndejembi.
Aidha ameongeza kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli Wilaya anayoiongoza ya Kongwa imeletewa zaidi ya Shilingi Bilioni sita kwa ajili ya miradi ya maji vijijini, mtandao wa barabara ya lami unaogharimu Bilioni tano pamoja na mradi wa maji Kongwa ambao kiasi cha Shilingi Bilioni 1.7 kilitengwa kufanikisha mradi huo wenye lengo la kumtua Mama ndoo kichwani.
” Ninapoona mtu analalamika ninashangaa sana, ndani ya kipindi cha miaka minne yamefanyika mambo makubwa ambayo kwa muda mrefu yalishindikana, uwekezaji mkubwa umefanyika kwenye nishati na umeme ambapo mradi mkubwa wa Stiglers unajengwa, umeme umefika hadi kijijini na kule kukatika katika kwa umeme migao ya mara kwa mara imekwama.
” Rais Magufuli ameimarisha miundombinu ya barabara Nchi nzima, lami imetandazwa kwenye kila barabara lengo, sekta ya afya imepiga hatua sana tunapozungumza hivi sasa vituo vya afya vinajengwa Nchi nzima, hakika Mhe Rais anastahili kupongezwa,” amesema DC Ndejembi.
Amempongeza Rais Magufuli kwa kusimamia nidhamu kwa watumishi wa umma huku pia akiongoza mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya.
” Hakuna mtu asiyejua namna ambavyo ilikua ngumu kuzuia biashara ya dawa za kulevya, lakini chini ya Rais Magufuli dawa za kulevya zimetokomezwa na ameaokoa kundi kubwa la vijana ambalo lilikua limeangamia kwa utumiaji wa dawa za kulevya.
” Sisi vijana tulioamiwa na Mhe Rais tuna jukumu zito la kumsaidia kazi, kutekeleza Yale yote ambayo amekua akihitaji kuona Watanzania wanyonge wananufaika na Nchi yao lakini pia ndani ya Chama chetu cha CCM tuko imara chini ya Mwenyekiti wetu Dk John Magufuli, ” Amesema DC Ndejembi.
Amewataka vijana na viongozi walioko ndani ya CCM kushikamana na kumuunga mkono Rais Magufuli ambaye tangu aingie madarakani ametekeleza kwa kiwango kikubwa ahadi yake ya elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.