Home Mchanganyiko ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA WIZI WA MTOTO MKOANI MBEYA

ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA WIZI WA MTOTO MKOANI MBEYA

0

***************

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja ANNA
EZEKIA [23], mkazi wa Itumbi Chunya na Igamba Wilayani Mbozi kwa
tuhuma za wizi wa mtoto.

Tukio hilo limetokea tarehe 21.07.2019 saa 09:30hrs Kijiji cha Itumbi, Kata
ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya.

Kufuatia tukio hilo Polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanya msako na
kufanikiwa kumpata mtoto huyo ANJELA ANJELY [miezi 9], akiwa hai
tarehe 22.07.2019 majira ya saa 07:00hrs akiwa ametelekezwa porini peke
yake Kitongoji cha Mwamapuli, Kijiji cha Mkola. Mtoto amefanyiwa uchunguzi
wa afya Hospitali ya Wilaya ya Chunya na hali yake ni nzuri.

Mtuhumiwa alikuwa na mazoea na mama mzazi wa mtoto huyo na alikuwa
anamtembelea mara kwa mara. Taratibu za kisheria zinafanywa ili afikishwe
Mahakamani.

KUPATIKANA NA BANGI:

Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia DENIS ABELI [35], mkazi wa
Usongole – Nsalala akiwa na bhangi uzito wa kilo 1 na gramu 200.

Tukio hilo limetokea tarehe 22.07.2019 saa 13:10hrs Kitongoji cha Usongole,
Kijiji na Kata ya Nsalala, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya kipolisi Mbalizi.

Mtuhumiwa ambaye ni muuzaji na mtumiaji wa bhangi, alificha bangi hiyo
kwenye begi lake dogo. Taratibu za kisheria zinafanywa ili afikishwe
Mahakamani.

KUPATIKANA NA SILAHA [GOBOLE] BILA KIBALI.

Mtu mmoja MAIKO WATSON [25], mkazi wa Kasasya alikamatwa nyumbani
kwake na Polisi akiwa anamiliki bila kibali silaha [gobole] mbili
zilizotengenezwa kienyeji zisizokuwa na namba.

Tukio hilo limetokea tarehe 22.07.2019 saa 07:45hrs Kijiji cha Kasasya,
Kataya Mtanila, Tarafa Kipembawe, Wilaya ya Rungwe. Aidha mtuhumiwa
alikutwa pia akiwa na risasi za gobole 53, fataki 7 pamoja na unga wa
baruti kwenye kopo moja. Mtuhumiwa ni muwindaji haramu.

WITO WA KAMANDA:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi ULRICH O. MATEI anatoa wito kwa wazazi / walezi kuwa na uangalizi
wa karibu na makini dhidi ya watoto katika himaya zao ili kuepuka matatizo
yanayoweza kuepukika.

Aidha Kamanda MATEI ameiasa jamii kutoa taarifa katika mamlaka husika
dhidi ya mtu / kikundi / mtandao wa watu wanaojihusisha na ujangili ili hatua
za kisheria zichuliwe dhidi yao. Pia ametoa wito kwa jamii hasa vijana
kuepuka kutumia dawa za kulevya kwani ni kinyume cha sheria na hatari kwa
afya zao.