Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali, akizungumza na wananchi na waumini wa dini, kwenye maadhimisho ya miaka 80 ya kanisa hilo, Julai 21.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipokea ngao kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli, kutoka kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali, kwenye maadhimisho ya miaka 80 ya kanisa hilo, yaliyofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, Julai 21.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***********
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelipongeza Kanisa la Tanzania Assemblies of God kwa kuthamini na kutambua kazi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano.
“Baba Askofu Mtokambali umenifurahisha kwa takwimu ulizozitaja hapa za miradi mikubwa ambayo inatekelezwa na Serikali hii. Kuna wengine hawapendi kusikia mambo kama haya, hongera sana,” amesema.
Ametoa pongezi hizo leo mchana (Jumapili, Julai 21, 2019) wakati akizungumza na maelfu ya waumini wa kanisa hilo katika maadhimisho ya miaka 80 ya TAG hapa nchini yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli, amesema ameguswa na jinsi kanisa hilo linavyomtambua Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake na kuthamini juhudi za Serikali.
“Serikali hii imedhamiria kuwatumikia Watanzania wote bila kujali dini zenu, rangi wala itikadi za kisiasa. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya awamu ya tano itaendelea kumtegemea Mungu pasipo shaka yoyote.”
Pia amewapongeza viongozi wa kanisa hilo kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka 80. “Pia nikupongeze Baba Askofu kwa kuchangia mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari hapa Arusha. Natambua kwamba ulishachangia mifuko mingine 500, asante sana.”
Alilishukuru kanisa hilo kwa kuendesha maombi maalum kwa ajili ya Taifa yaliyoongozwa na Mchg. Titus Mkama. “Niliguswa sana wakati maombi ya Taifa yalipokuwa yakiendelea. Mchungaji aligusia masuala ya muhimu kwa Taifa hili.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na maelfu ya washirika waliohudhuria maadhimisho hayo, Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali alisema anamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kulipenda na kulijali kanisa hilo.
Alimpongeza Rais Magufuli kwa miradi mikubwa ya maendeleo anayoisimamia kama vile umeme wa Stiegler’s Gorge, reli ya SGR, ununuzi wa ndege, ujenzi wa hospitali mpya 67 za wilaya, ujenzi wa vituo vya afya 370 na ununuzi wa dawa za hospitali.
“Nina umri wa kutosha lakini katika miaka yangu yote hii, sijawahi kuona hospitali 67 zikijengwa kwa pamoja. Tena, mwaka huu wa fedha mmetenga hela kwa ajili ya ujenzi wa hospitali nyingine 27. Hongera sana kwa ujasiri huo,” alisema Dkt. Mtokambali.
Maadhimisho ya miaka 80 ya TAG yameenda sambamba na hitimisho la miaka 10 ya Mpango Mkakati wa mavuno.