Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Bwana Pereira Silima akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mlele Rachel Kasanda mara baada ya kuwasili wilayani humo
Baadhi ya Vijana wanaotengeneza barabara ya Mpanda Tabora kwa kiwango cha lami wakimshangilia Kiongozi huyo baada ya kuusimamisha msafara wake
Sehemu ya ujenzi wa jengo mojawapo katika hospitali ya Wilaya ya Mlele
Wajumbe wa mashina wa kijiji cha Kamsisi wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa CCM mikoa ya katavi na Rukwa Pereira Silima
……………………….
Na Mwandishi wetu Katavi
Vijana wanaotengeneza barabara ya Mpanda – Tabora kwa kiwango cha lami walioajiriwa na kampuni ya ukandarasi ya kichina ya CRSG; waliokuwa katika eneo la Ikonda Moyo katika halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi wameusimamisha msafara wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Pereira Silima ambaye pia ni mlezi wa Chama cha Mapinduzi kwa mikoa ya Katavi na Rukwa; kwa lengo la kumshukuru Rais kwani kupitia mradi huo wa miaka mitatu wameweza kupata ajira
Vijana hao wamesema wamefanya hivyo ili kumfikishia ujumbe Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli na kuongeza kuwa mradi mkubwa kama huo umeokoa vijana wengi waliokuwa hawana ajira na hivyo kuwaepusha kushiririki vitendo vya uhalifu
“Kwakweli mradi huu unasaidia vijana wengi, watu tumetoka maeneo mbalimbali mi mwenyewe nimtoka Dar es Salaam, wapo watu kutoka Singida, Tabora na hata Katavi yenyewe” alisema Kasim Juma mmoja wa wafanyakazi katika Mradi huo
Bwana Silima yuko mkoani Katavi kwa ziara ya kuboresha mashina ya Chama cha Mapinduzi sanjari na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali
Kwa upande wake Silima amesema kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa imezaa matunda mengi
Naye Katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Katavi bwana Jackson Lema amewataka vijana kumuunga mkono Rais kwa kuchapa kazi
Awali Katibu huyo wa Halmashauri Kuu ya Taifa alikagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mlele ambayo ilikuwa imesimama ujenzi kwa zaidi ya mwezi mmoja kutokana na mkandarasi kuchapisha matofali ya chini ya kiwango
Akitoa taarifa ya ujenzi huo Mkuu wa Wilaya ya Mlele Bi. Rachel Kasanda amesema zaidi ya matofali elfu themanini yalikuwa hayafai hali iliyolazimisha kutafuta mkandarasi mwingine na kuchapisha upya matofali mengine
Aidha kwa sasa ujenzi wa hospitali hiyo uko katika hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuinua maboma wakati majengo mengine yakiwa yanashindiliwa udongo
Kuhusu ujenzi huo Silima amewashauri kuongeza nguvu ili kuendana na kasi ya serikali kwani kukamilika mapema kwa hospitali hiyo kutatoa fursa kwa wananchi kupata huduma