Kiongozi wa timu hiyo ya wataalamu wa utafiti , Bw. Saleh Pamba.
Eneo la Bonde la Mto Rifiji ambako mradi huo unatekelezwa.
……………………………………………………
TIMU ya wataalamu bingwa watano wa kitanzania waliobobea katika masuala ya uhifadhi, mazingira na uchumi, juzi ilizindua ripoti yake ya utafiti wa kitalaamu kuhusu faida na madhara ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme wa Mto Rufiji, unaofahamika zaidi kama Stiegler’s Gorge Hydropower Project.
Ripoti hiyo imezinduliwa zikiwa zimesalia takriban siku saba kabla ya kuzinduliwa rasmi kwa ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na Kampuni inayomilikiwa na Serikali ya Misri,inayofahamika kwa jina la Arab Contractors.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Hotel ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam, kiongozi wa timu hiyo wa wataalamu, Saleh Pamba alisema utafiti wao ulilenga kuangalia madhara na faida za ujenzi wa mradi baada ya mashirika mawili ya umoja wa mataifa kujitokeza hadharani kupinga azma ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, kuutekeleza.
Pamoja na Pamba, wataalamu wengine katika timu hiyo ni Dk. Abubakar Rajab, Abdulkarim Shah, Dk. Magnus Ngoile na Dk. Thomas Kashililah.
Pamba aliyataja mashirika ya umoja wa mataifa yaliyojitokeza kuupinga mradi huo na kusambaza taarifa zake duniani kote zikieleza athari zitakazojitokeza iwapo utatekelezwa kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF).
Alisema hoja za upinzani huo dhidi ya uamuzi wa Rais Dk. Magufuli zilizosambazwa duniani kote kwa njia ya maandishi kwenye vyombo vya habari na mitandao mbalimbali ya kijamii kabla ya kubebwa na baadhi ya wapinzani wa maendeleo wa ndani ya Tanzania zilianza kujenga taswira mbaya dhidi ya mradi wenyewe na Rais Magufuli ambaye aliapa kuutekeleza.
“UNESCO na WWF walitushtua sana baada ya kusoma maandiko yao yaliyokuwa yakipinga mradi wa Stiegler’s, waliandika hoja nyingi zilizokuwa zikipinga uamuzi wa rais kutekeleza ujenzi wa mradi huo wakitaka jumuiya ya kimataifa ipaze sauti kwa pamoja ili usitekelezwe. Sisi tulishtuka kwa sababu hizo hoja zao nyingine zilikuwa haziingii akili lakini nyingine zilikuwa zinafikirisha.
“Tukaona kama wasomi wa kitanzania ni wajibu wetu kujiridhisha ili kama kuna hizo hatari walizozianisha tuishauri serikali ifanye vinginevyo, tumefanya utafiti wa kina kweli kweli, tumegusa kila kipengele walichopigia kelele lakini sasa ajabu tulichogundua ni kwamba kelele zote za hao wazungu ni uongo mtupu. Wanatishwa na kasi ya Rais Dk. Magufuli kuliletea maendeleo taifa letu,” alisema Pamba.
Alisema, haina shaka hata kidogo kuwa mataifa ya Magharibi yanajaribu kutumia kisingizio kuwa Hifadhi ya Selous ambayo inatambulika kama eneo la urithi wa dunia na mahali unapojengwa mradi wa Stiegler’s, serikali imekusudia kupaharibu lakini ukweli ni kwamba hofu kubwa ya Magharibi ni kasi ya Tanzania kuelekea kwenye uchumi wa kati na kujitoa kwenye utegemezi wa mataifa hayo na taasisi zake za misaada.
Pamba alisema katika utafiti wao wamebaini kuwa eneo la hifadhi la Selous litakalotumika kujenga mradi ni asimilia mbili tu ya kilomita za mraba 50,000 hivyo sehemu kubwa ya hifadhi haitaguswa na kwamba hata eneo ambalo mradi utatekezwa halitaathirika na uharibifu wa mazingira au kuhatarisha ustawi a wanyama.
“Kama UNESCO na WWF wana wasomi wasiokuwa na uwezo wa kufanya utafiti wa kiwango kile basi tafiti zao hasipaswi kupewa kipaumbele hata siku moja. Lakini sisi katika utafiti wetu tulibaini kuwa hawa jamaa ajenda yao ni kuhakikisha Tanzania haifikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo 2025.
“Umeme wa Stiegler’s utawezesha kukua haraka kwa sekta za viwanda, madini, uendeshaji wa treni za kisasa ya umeme, upatikanaji wa umeme vijijini na wafanyabiashara wadogo watakuwa na uhakika wa kupata umeme wa bei nafuu, uchumi wetu utapaa kwa kasi ya ajabu.
“Ripoti yetu hii ambayo tunaitoa kwenu waandishi wa habari nendeni mkaisome na mtakubaliana na sisi kuwa uamuzi wa ujenzi wa mradi huo ulifikiwa miaka 60 na 70 huko lakini uamuzi wa kuifanya Selous kuwa eneo la urithi wa duniani ulichukuliwa mwaka 1982. Hizi taasisi za kimataifa zilikuwa na taarifa kuhusu uamuzi wetu huo.
“Sasa katika hoja zao za sasa wanasema ujenzi wa mradi huo utahatarisha hali ya usalama na utasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, siyo kweli hata kidogo. Sisi tumebaini katika utafiti kuwa utekeklezaji wa mradi utalinda mazingira na tumefafanua vizuri sana katika ripoti kuwa hali ya usalama itamaarika mno kwa sababu kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika eneo zima la mradi hivyo hata wawindaji haramu hawatasogolea huko.
“Hawa wazungu wanasema wakati wa utekelezaji wa mradi kutakuwa na kelele na uchafuzi wa hewa, hoja za kitoto kabisa kwa sababu sisi katika uchunguzi wetu tumebaini kuwa kabla ya mradi kuanza kutekelezwa, hivi sasa kuna viwanja vya ndege vidogo, hizi Airstrips 38 na kati za hizo 33 zinafanya kazi kila uchao kusafirisha watalii, hapo hawaoni kelele hizo za ndege kupaa na kutua.
“Sasa utafiti hupingwa kwa utafiti, ripoti ya utafiti wetu tumeiweka mezani kama wao wanayo yao mpya ya utafiti wa kweli kweli siyo ya kuchafua nchi au rais nao waiweke mezani. Wapeni watanzania ripoti yetu wajue kuwa mradi huu una manufaa makubwa kwa nchi yetu na hawa wazungu lengo lao tusiutekeleze ili tuendelee kuwategemea wao.
“Kwetu sisi tunaiomba serikali ichukue hatua madhubuti za ujenzi wa vyanzo vipya vya uzalishaji umeme wa uhakika ili iepuka kushindwa kufikia malengo ya kuwa taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Pia Tanzania inapaswa kuwa na vyanzo vipya vya umeme wa uhakika ili kuepuka hatari ya maeneo ya misitu kugeuka jangwa na kuepuka athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, alisema Pamba.
Alisema kupatikana kwa umeme wa uhakika kutaepusha uteketezwaji wa kilimota za mraba 412,000 za misitu kila mwaka kwa ajili ya shughuli za kibinadamu na hivyo kuongeza ustawi wa maeneo ya uoto wa asili na mapori mengi zaidi.