Baadhi ya madereva bodaboda wa Manispaa ya Mpanda wakiwa katika Mkutano na Waandishi wa Habari
Emmanuel Minazi Mwenyekiti wa waendesha Bodaboda Mpanda
Baadhi ya pipipiki zilizokuwa zimepaki nje ya ukumbi wa Garden Mpanda wakati mkutano ukiendelea ndani
…………………….
Na Mwandishi wetu Katavi
Madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda wa manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wamemlalamikia Mkuu wa wilaya hiyo kwa kuwalazimisha kukata vitambulisho vya wajasiriamali
Wakizungumza na waandishi wa habari madereva hao wamedai kuwa mkuu huyo wa wilaya anawatishia kuwa ana jeshi kubwa hivyo wakikaidi atawakamata na kuwalaza lupango
Wamesema si kwamba wanakataa kumuunga mkono mheshimiwa Rais bali wanaona wanaonewa kwani kama ni kodi tayari wanachangia kila kukicha katika ununuzi wa mafuta licha ya vibali vingine vinavyowapasa kuwa barabarani kama mapato ya TRA na SUMATRA
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa waendesha Bodaboda mkoa wa Katavi Emmanue Minazi amekifananisha kitendo cha kukatishwa kitambulisho cha wajasiriamali kwa bodaboda kuwa sawa na dhambi kubwa
“Mkikubali kukata kitambulisho cha wajasiriamali mimi najiuzulu nafasi yangu” alisema Minazi
Bwana James Sunga ni mmoja wa madereva wa bodaboda katika manispaa ya Mpanda, amesema wao ni madereva kama walivyo madereva wengine hivyo haoni ni kwanini tamko hilo limewaangukia madereva bodaboda pekee
Aidha wamemwomba mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kufanya ziara mkoani Katavi kwa madai kuwa wana kero nyingi sana za manyanyaso na uonevu kutoka kwa viongozi mbalimbali
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mpanda mama Lilian Matinga amefafanua kuwa agizo hilo ni kwa madereva wote ambao si wamiliki wa vyombo vya moto na wala sio kwa madereva wa pikipiki peke yao; ili kuichangia serikali mapato
Mama Matinga amesema kuwa waliitisha kikao na madereva wote wa mkoa wa Katavi wakiwemo madereva wa Bajaji, Kirikuu na Mabasi na kwamba waliomba kupewa muda ili kuvilipia vitambulisho hivyo kidogo kidogo jambo ambalo kama wilaya waliridhia
Ameongeza kuwa kupitia kodi mbalimbali miradi mbalimbali inatekelezwa na hivyo kuwataka Bodaboda kuachana na ukaidi na kulipia vitambulisho vya wajasiriamali