Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ambaye
amemwakilisha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack
Kamwelwe, akihutubia Viongozi wa Serikali na wadau wa Sekta ya Ujenzi
waliohudhuria katika warsha ya utambulisho wa mradi wa ujenzi wa barabara ya
Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) sehemu ya Tanzania na Rumonge-Gitaza (km
45) sehemu ya Burundi kwa kiwango cha lami uliofanyika mkoani Kigoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale,
akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km
260) kwa kiwango cha lami utakaoanza hivi karibuni. Ujenzi wa barabara hiyo
utagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo
ya Afrika.
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Alex Mubiru,
akizungumza na Viongozi wa Serikali na wadau wa Sekta ya Ujenzi
waliohudhuria warsha ya utambulisho wa mradi wa ujenzi wa barabara ya
Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) sehemu ya Tanzania na Rumonge-Gitaza (km
45) sehemu ya Burundi kwa kiwango cha lami uliofanyika mkoani Kigoma.
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi
na Mawasiliano) ambaye ni Mbunge wa jimbo la Muhambwe, Mhandisi Atashasta
Nditiye (kulia), akiteta jambo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.
Joyce Ndalichako (kushoto), katika warsha ya utambulisho wa mradi wa ujenzi
wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) sehemu ya Tanzania na
Rumonge-Gitaza (km 45) sehemu ya Burundi kwa kiwango cha lami uliofanyika
mkoani Kigoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akiwa katika
picha ya pamoja na viongozi wengine wa Serikali pamoja na wadau wa Sekta ya Ujenzi kutoka nchi ya Tanzania katika warsha ya utambulisho wa mradi wa ujenzi
wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) sehemu ya Tanzania na
Rumonge-Gitaza (km 45) sehemu ya Burundi kwa kiwango cha lami uliofanyika
mkoani Kigoma.
Muonekano wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) kwa kiwango cha
lami utakavyokuwa mara baada ya ujenzi wake kukamilika, mkoani Kigoma.
Ujenzi wa barabara hiyo utajumuisha miradi ya kijamii inayogusa moja kwa moja
wananchi katika Sekta ya Elimu, Maji na Afya.
*********
Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa
barabara ya Kabingo – Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilomita 260 Kwa
kiwango cha lami ikiwa ni hatua ya kuendelea kuufungua mkoa wa huo katika
miundombinu ya barabara mkoani Kigoma.
Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuwa wa muda
mfupi kutokana na kugawanywa katika sehemu nne ambazo ni Manyovu – Kasulu
(km 68.25), Kanyani – Mvugwe (km 70.5), Mvugwe – Nduta (km 59.35) na Nduta
– Kabingo (km 62.50).
Akizungumza katika hafla ya kuutambulisha mradi huo mkoani humo kwa
viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa, wadau wa Sekta ya Ujenzi na Wabunge,
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale,
amesema tayari Serikali imepata fedha za mkopo wa nafuu kutoka Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba
kazi inayoendelea hivi sasa ni kukamilisha taratibu za kumpata mzabuni.
"Mpaka sasa zabuni ya mradi wa barabara hii imeshatangazwa na ujenzi utaanza
hivi karibuni mara baada ya taratibu nyingine kukamilika", amesisitiza Mhandisi
Mfugale.
Amebainisha kuwa mradi huu ni wa mfano kwani utahusisha miradi mingine ya
kijamii inayogusa moja kwa moja wananchi katika Sekta ya Elimu, Maji na Afya.
Ametaja miradi hiyo kuwa ni Ukarabati wa masoko ya Makere na Manyovu,
Ujenzi wa Sekondari ya Buhigwe na Shule ya Msingi Busunzu, Ujenzi wa vituo
vya mabasi vya Manyovu na Kabingo, Kusambaza maji katika maeneo ya
Busunzu, Kasulu, Buhigwe na Manyovu, Uboreshaji wa kituo cha Afya cha
Makere, Ununuzi wa magari manne ya Wagonjwa (Ambulance) na Ukarabati wa
Hospitali ya Kasulu na Kibondo.
Akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amesema kuwa
mradi huo ni moja ya miradi mikubwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
utakaosaidia kuinua uchumi wa nchi sambamba na kuunganisha mkoa wa
Kigoma na mikoa mingine pamoja na nchi jirani.
"Mradi huu utaandika historia mpya katika nchi ya Tanzania kwani ni moja ya
barabara pekee inayounganisha nchi yetu na nchi jirani iliyokuwa imebaki katika
kiwango cha changarawe", amesema Prof. Ndalichako.
Ameongeza kuwa utaratibu wa kuwafahamisha wadau na wananchi kuhusu ujio
wa miradi utasaidia kutatua changamoto zitakazojitokeza na kupata ushirikiano
wa karibu wa maoni ambayo yatawezesha kufanikisha utekelezaji wa mradi huo
ndani ya muda, gharama na ubora unaotakiwa.
Naye Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Alex
Mubiru, ameeleza kuwa Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuhakisha
kuwa miradi hiyo inakuwa chachu ya kukua kwa uchumi na kupunguza umaskini.
Ameongeza kuwa Benki imeweza kuandaa fedha za utekelezaji wa miradi
mikubwa mitatu (3) ambayo ni ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu
(km 260), Dodoma Outer Ring (km 110.2) na ujenzi wa barabara Tanga –
Pangani – Bagamoyo (km 121) ikiwa ni lengo la kufungua fursa mbalimali za
maendeleo nchini Tanzania.
Warsha hiyo ya siku mbili yenye lengo la kuwafahamisha wadau mbalimbali
kuhusu mradi huo imehusisha Mawaziri na Wabunge wanaotoka eneo la mradi,
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa
Wilaya zilizopo mkoani humo, Maafisa Watendaji wa Misitu, Madini, Ardhi, Shirika
la Umeme (TANESCO), Maji na Shirika la Mawasiliano (TTCL).