Home Mchanganyiko WANANCHI WAUNDA VIKUNDI KAZI KUTOKOMEZA VIFO VYA WAJAWAZITO

WANANCHI WAUNDA VIKUNDI KAZI KUTOKOMEZA VIFO VYA WAJAWAZITO

0

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela chilumba hivi karibuni akiwahutubia wakazi wa kata ya Mtipwili katika Uzinduzi wa kampeni ya” Jiongeze Tuwavushe” yenye lengo la kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto kwa kuhakikisha kila mama mjamzito anapata huduma ya afya katika kiyuo cha afya wilayani Nyasa([picha na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Nyasa).

*************

Wananchi wa kata ya Mtipwili Wilayani Nyasa, wameunda vikundi shirikishi vya
kuwafichua akina mama wajawazito, wasiohudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya na uzazi ili kuzuia vifo vya akina mama wajawazito na watoto.

Hayo yameelezwa na Mganga mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Dkt Aron Hyera wakati akitoa Taarifa kwa Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Bi isabela Chilumba, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Jiongeze Tuwavushe salama”, uliofanyika jana katika viwanja vya mikutano vilivopo katika kijiji cha chiulu,Kata ya Mtipwili Wilayani hapa. Kampeni yenye lengo la kutokomeza vifo vya akina mama wajawazito na watoto.

Dkt.Hyera alifafanua kuwa, kampeni ya “Jiongeze tuwavushe salama” ina lengo la
kutokomeza vifo vya akina mama waja wazito na watoto vinavyotokana na matatizo ya uzazi na wamelazimika kuzindua kampeni hiyo yenye lengo la kuipa elimu jamii ijue kuwa kila mama mjamzito anapohisi dalili za ujauzito anatakiwa kuwahi kuja katika kituo cha kutolea huduma za Afya zilizo karibu ili, kutokomeza vifo hivyo.

Aliongeza kuwa, wamelazimika kuzindua kampeni hiyo katika kata ya Mtipwili, kwa
kuwa ni moja ya Kata zilizoathirika na vifo vya akina mama wajawazito. kwa kipindi cha miaka mitatu, vimetokea vifo viwili (2)vya akinamama wajawazito waliopoteza maisha kwa kuchelewa kufika, katika vituo vya kutolea huduma. Kwa kuona hali hiyo wameamua kuwashirikisha wanajamii ili wachukue hatua kwa wazazi/walezi wanaochelewa kwenda katika vituo vya kutolea huduma vilivyopo katika maeneo yetu.

“Katika Kata hii ya Mtipwili tumeunda vikundi vya kuhamasisha wanajamii na
kuhakikisha kuwa, kila mama mjamzito anaanza kliniki mapema ili kutokomeza vifo
vinavyotokana na uzazi. kuwaelimisha wanajamii wote, kuwa kila mama anayehisi dalili za ujazito anaenda mapema katika kituo cha kutolea huduma za afya ili kutokomeza vifo vya uzazi. Tunataka kupiga vita vifo hivyo kwa kuwa Serikali yetu imetuboreshea huduma za afya katika Wilaya yetu kwa kutujengea Hospitali Mpya ya Wilaya ya Nyasa, vituo vya afya Mkili na Kihagara ili tuwe na afya nzuri na tufanye kazi kwa juhudi na vikundi kazi hivi vimefanya kazi nzuri na akina mama wote wanahudhuria katika vituo vya kutolea huduma.” alisema Dkt hyera.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Bi Isabela Chilumba akihutubia wananchi wa kata ya Mtipwili aliwapongeza kwa kuanzisha vikundi kazi hivyo na kuwataka kuwathamini akinamama wajawazito na kupiga vita vifo vinvyotokana na uzazi katika wilaya hii, kwa kuwafikisha mapema wajawazito wote katika vituo vya afya na kuwachukulia hatua kali wale wote ambao hawatatoa ushirikiano katika jamii.

Aidha alimwagiza Mganga mkuu Dkt Aroin Hyera kuhakikisha kuwa Kata zote za Wilaya ya Nyasa zinakuwa na vikundi kazi hivyo na kuhakikisha vinafanya kazi ya kuhamasisha jamii juu ya akina mama wajawawazito kujiunga na huduma hizo mara wajisikiapo kuwa na dalili za ujauzito.

“Nakuagiza mganga mkuu wa wilaya ya Nyasa, hakikisha kuwa kila Kata iwe na vikundi shirikishi na viwe vinafanya kazi ya kuwaelimisha,kuhamasisha wanajamii katika wilaya ili kutokomeza vifo vya akina mama wajawazito na watoto na kuwachukulia hatua kwa wale wote wasiohudhuria katika vituo vya kutolea huduma mapema.

Nao wananchi wa Kata ya Mtipwili walipongeza uongozi wa Wilaya kwa kufanyia
uzinduzi katika kata ya Mtipwili na kutoa elimu hiyo, na waliahidi kutokomeza vifo hivyo kwa kuhakikisha kila mama Mjamzito anahudhuria katika kituo cha afya mapema.

“Mkuu wa wilaya yetu tunakupongeza sana kwa kazi zako nzuri za kutuletea maendeleo katika Wilaya yetu ya Nyasa na kuchagua Mtipwili kufanyia uzinduzi wa kampeni hii ya Tuwavushe salama,kwetu sisi ni faraja sana na tunakuhakikishi tutatokomeza vifo hivyo katika kata yetu” alisema Diwani wa Kata ya Mtipwili Richard Chialo wakati akifunga shughuli za uzinduzi.