Mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, Azam FC leo Jumanne Julai 16, 2019 imetinga nusu fainali baada ya kuitoa TP Mazembe kwa kuifunga mabao 1-2, huku mshambuliaji Eliud Ambokile akicheza kwa mara kwanza katika kikosi cha mabingwa hao wa DR Congo.
Mshambuliaji Obrey Chirwa amethibisha ubora wake baada ya kufunga bao la ushindi kwa Azam iliyolazimika kutoka nyuma kabla ya kuibuka na ushindi huo licha ya Mazembe kuonyesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira pamoja na kushambulia kwa umakini.
Mazembe walianza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Ipyamy Giovani dakika 21, lakini goli hilo lilidumu kwa dakika saba tu baada ya Idd Seleman ‘Nado’ kusawazisha kwa Azam katika dakika 28.
Katika kipindi cha kwanza Mazembe walikuwa wakimiliki mpira kuzidi Azam baada ya kupiga mashuti matatu golini kwa Azam huku Azam wakiwa hawajapiga shuti mmoja tu.
Mazembe walikuwa wakishambulia kuliko Azam kiasi ambacho kiliwafanya kupata kona tano ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza huku Azam wakiwa hawajapata kona yoyote ile.
Katika kipindi cha pili Azam ilifanya mabadiliko dakika 57 kwa kumtoa Donald Ngoma na kuingia Paul Peter ili kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji, Ngoma alionekana kukamatwa na mabeki wa Mazembe.