Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, akizungumza katika uzinduzi wa Ilala ya Kijani.
Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Tabia Mwita akiwa ameshika zawadi ya picha ya Rais Dk. John Magufuli.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, akiendesha mnada wa keki ambayo ilinunuliwa kwa Sh milioni 1.8 Kulia ni mgeni rasmi Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Tabia Mwita.
************
NA MWANDISHI WETU
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema kuwa sasa unajipanga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa kuhakikisha unampatia kura za heshima Rais Dk. John Magufuli.
Pamoja na hali hayo, UVCCM imesema ni vema chama kikatoa fursa kwa vijana kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kama njia ya kumuenzi Rais Magufuli ambaye ameamua kuwaamini katika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.
Akizungumza Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Ilala ya Kijani, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema wao kama vijana kwa sasa wanatembea kifua mbele kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli pamoja na wasaidizi wake, wakiwamo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na mawaziri.
Kilakala amesema viongozi hao wamekuwa wakijenga heshima kwa nchi na chama kwa kuhakikisha wanasimamia falsafa na misingi ya CCM kwa kuimarisha mshikamano kwa Watanzania.
“Ndugu Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa (Tabia Mwita), sisi vijana wa Dar es Salaam tunatembea kifua mbele kwani Rais Magufuli amekiheshimisha chama na taifa letu kwa ujumla na mwaka 2020 tutampatia kura za heshima.
“Lakini pia kama kiongozi wa nchi (Rais Magufuli), ameweza kuwaamini vijana basi na uchaguzi wa mwaka huu tunakiomba chama kitoe tamko la kutokata majina ya wagombea vijana ambao muda wote wamekuwa wakikijenga chama kwa kuimba ‘hiyena hiyena’ na sasa nao waweze kuingia katika uongozi wa Serikali za Mitaa, udiwani na hata ubunge,” amesema Kilakala.
Mgeni rasmi katika mkutano huo wa ndani, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Tabia Mwita, amesema kuwa ili kijana aweze kutimiza wajibu wake, ni lazima ahahakikishe anajiandikisha na kuwa na kitambulisho cha kupigia kura.
Tabia alisema hatua hiyo itahakikisha ushindi mnono wa CCM kwa kushinda viti vya mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Amesema agizo la CCM ni kuhakikisha inashinda nafasi zote za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Serikali Kuu.
“Kama kuna mtendaji yeyote atakayekwamisha uandikishaji kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura toeni taarifa haraka ili tumpe taarifa Mwenyekiti wa CCM Rais John Magufuli,” amesema Tabia.
Pia ametoa onyo kwa mataifa yanayojaribu kuisemea demokrasia ya nchi na kuwataka watatue matatizo yanayowakabili badala ya kushughulika na Tanzania.
Pia aliwataka viongozi wa chama hicho kushirikiana na kuepuka migogoro ya ndani inayokigawa chama hicho kipindi cha uchaguzi.
“Tuacheni tabia za kubomoana wenyewe kwa wenyewe, tunahitaji ushirikiano na muelekezane kwa utaratibu uliowekwa na chama,” amesema Tabia.
Mwenyekiti wa UVCCM, Wilaya ya Ilala, Amani Pazi, amesema wamefanya uchunguzi na kubaini kwamba asilimia 80 ya wapigakura ni vijana, hivyo ili kuweza kushinda uchaguzi wagombea vijana wapewe kipaumbele zaidi.
Katika mkutano huo, wanachama 200 walijiunga na CCM akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) upande wa Vyuo Vikuu, Jackson Nzinza.