Diwani wa kata ya Mwangata katika Halmashauri ya manispaa ya Iringa Nguvu Chengula akiwa amepiga magoti kuomba wanachama wa vikundi vya ujasiliamali vya umoja wa wanawake Tanzania (UWT) kata ya Mwangata kusaidia CCM kushinda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa jana wakati wa uzinduzi wa vikundi hivyo ukumbi wa damu ya Yesu Mwangata (picha na Francis Godwin)
***************
Diwani Chengula alisema kwa ajili ya kuviwezesha vikundi hivyo kusajiliwa katika Halmashauri tayari mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Rose Tweve ( CCM) amevitembelea vikundi vya kata ya Mwangata na kuvisaidia fedha kiasi cha shilingi 500,000 kwa ajili ya kukuza mitaji huku yeye kama diwani wa kata ameviongeza kiasi cha shilingi 800,000 ili kuviongezea nguvu ya kusajiliwa kisheria.
“ Serikali ya chama cha mapinduzi (CCM) chini ya mwenyekiti wetu Rais Dkt John Magufuli ipo kuona wananchi wenye sifa ya kupewa mikopo hii wananufaika nayo na mikopo hii haitakiwi kurejeshwa kwa riba yoyote hivyo ni haki ya kila mwenye sifa kupewa mikopo hiyo iwapo atakuwepo kwenye kikundi “ alisema Chengula
Hivyo alisema fedha hizo ni haki ya makundi husika na lazima Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutoa mikopo hiyo kwa makundi hayo bila kuwepo kwa ubaguzi wowote iwapo vikundi vitakuwa vimetimiza sifa zinazohitajika .
“ Mimi kama diwani wenu nitahakikisha napambana kuubana uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Iringa ili fedha hizo ziweze kutolewa kwa vikundi vyote ambavyo vitakuwa vimetimiza sifa ya kupewa mikopo hiyo na sitakubali kuona mnahangaika kutafuta mitaji wakati fedha za serikali zipo “ alisema Chengula
Kuwa vikundi vya kata hiyo vimekuwa mfano wa vikundi vingine ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kutokana na aina ya shughuli za uendeshaji wa viwanda vidogo vidogo vya utengenezaji batiki na vikapu vya kisasa ambavyo wanachama wake wamekuwa wakifanya na shida yao ni mitaji ya kuboreshea huduma zao.
Naibu meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Joseph Ryata alisema kuwa uhakika wa vikundi hivyo kupewa mikopo upo na kutaka kukamilisha taratibu za usajili wa vikundi hivyo hasa vile ambavyo havijasajiliwa .
Aidha alisema wajibu wa halmashauri hiyo kuendelea kuwaunganisha wananchi wake na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo nafuu kama inayotolewa na shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO) mkoa wa Iringa .
Awali wanavikundi hao wakitoa changamoto zao wakati wa kikao hicho cha uzinduzi wa vikundi vya vya wajasiliamali kata ya Mwangata walisema changamoto kubwa ni Halmashauri kushindwa kutoa mikopo kwa wakati .