Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Civil Social Protection Foundation (CSP) Nemency Iriya akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati ya kupambana na vitendo vya ukeketaji.
Waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara, wakimsikiliza Mkurugenzi wa CSP, Nemency Iriya akizungumza nao juu ya mikakati ya kupambana na vitendo vya ukatili vya ukeketaji.
***************
KATIKA kupambana na ukeketaji ulioenea Mkoani Manyara, shirika lisilo la kiserikali la Civil Social Protection Foundation (CSP) limeanzisha mradi wa mwaka mmoja wa kubadili vikwazo vya kiutamaduni na kutokomeza vitendo hivyo.
Mkurugenzi wa CSP Nemence Iriya akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati alisema wameanzia wilayani Hanang’ kisha watafuata wilaya nyingine za mkoa huo.
Iriya alisema watawatumia wazee wa kimila wa eneo hilo katika kikao chao ili kuhakikisha wanatokomeza vitendo hivyo vya kikatili ambavyo mkoa wa Manyara unaongoza nchini kwa asilimia 58.
Alisema wameazimia kutumia mijadala kwa jamii ili kutokomeza vitendo hivyo kuliko kuwashurutisha kwani ni bora kubadili fikra zao wenyewe na kuongeza uelewa wa moja kwa moja.
“Ukeketaji umejikita kwenye kanuni na taratibu za kijamii, imani za utamaduni na vichocheo vya kiuchumi na unatumika kama njia ya kudhibiti ashki ya kujamiiana kwa wanawake,” alisema Iriya.
Alisema katika jamii nyingi inachukuliwa kama jambo la muhimu kwenye shughuli za jando na unyago na simulizi potofu za ukeketaji zimekuwa zinajirudia mara kwa mara.
Mwezeshaji wa mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia, Charles Odero alisema wamewajengea waandishi wa habari uwezo zaidi ili jamii izidi kufaidika kupitia vyombo vyao.
Odero alisema kupitia taarifa za waandishi hao jamii itazidi kupata uelewa wa madhara ya vitendo vya kikatili vya ukeketaji ambapo mkoa wa Manyara unaongoza kwa vitendo hivyo kwa hapa nchini.
Alisema waandishi hao wataeleza hali ipoje, nani anahusika, inasababishwa na nini, sheria, mipango, mikataba ya kimataifa inaelezeaje juu ya hayo na kusikiliza jamii pia ikizungumza juu ya hilo.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara, (Mamec) Mary Margwe alisema hivi sasa baada ya serikali kuongeza nguvu za kupambana na ukeketaji jamii imebadili mtindo kwa kuwakeketa watoto wachanga kwa kutumia kucha.
“Elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwa jamii ili kuhakikisha vitendo hivi vinamalizika kwani vimepitwa na wakati na wanapaswa kubadilika tofauti na miaka iliyopita,” alisema Margwe.
Kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukeketaji nchini, kumeelezwa kama eneo lenye kuleta wasiwasi wa utekelezaji wa mikataba ya haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.