Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia eneo la pembezoni mwa ziwa Victoria wilayani Magu mkoani Mwanza lenye ukubwa wa ekari 94.1 lililorejeshwa serikalini na Klabu ya Gofu ya Victoria, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt Josephat Sengati.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika eneo la pembezoni mwa ziwa Victoria wilayani Magu mkoani Mwanza ambapo Klabu ya Gofu ya Victoria imelirejesha Serikalini . Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt Josephat Sengati na wa pili kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Biswalo Misuse.
Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Magu Wilfred Mkono (Wa pili kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa kukagua eneo lenye ukubwa wa ekari 94.1 lililoko pembezoni mwa ziwa Victoria wilayani Magu ambalo limerejeshwa Serikalini. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
*********
Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
Klabu ya Golfu ya Victoria (Victoria Golfu Club) imetoa eneo lenye ukubwa wa ekari 94.1 liliko pembezoni mwa Ziwa Victoria wilaya ya Magu mkoa wa Mwanza kwa Serikali ikiwa ni kuunga mkoni jitihada za serikali ya awamu ya tano katika suala la uwekezaji.
Eneo hilo ambalo halmashauri ya wilaya ya Magu ililitengea matumizi ya ujenzi wa nyumba za makazi, Hoteli pamoja na matumizi mengine lina jumla ya viwanja saba vilivyokuwa vikimilikiwa na klabu ya Golfu ya Victoria.
Akizungumza wilayani Magu mkoa wa Mwanza jana alipotembelea eneo hilo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula aliishukuru Klabu ya Golfu ya Victoria kupitia Wakurugenzi wake kwa uamuzi wa kukubali kulitoa eneo hilo ambapo aliuelezea uamuzi huo kuwa ni wa kizalendo kwa nchi ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, eneo hilo la pembezoni mwa Ziwa Victoria linafaa sana kwa shughuli za uwekezaji na sasa litakuwa ni mali ya serikali baada ya wamiliki wake kukubalia kuikabidhi serikali na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi itakuwa na jukumu la kulipangia matumizi.
Akiwa ameambatana na KatibuMkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dorothy Mwanyika, Naibu Waziri Mabula alionya juu ya uvamizi au udanganiyifu wowote unaoweza kufanywa na wananchi wasiokuwa waaminifu na kusisitiza kuwa eneo hilo kwa sasa litakuwa chini ya Wiazara ya Ardhi mpaka hapo litakapopangiwa taratibu nyingine.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt Phelemon Sengati alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula kuwa wilaya yake itahakikisha eneo lililokabidhiwa linalindwa na hakuna mwananchi atakayeruhusiwa kufanya shughuli yoyote hadi hapo serikali itakapokuja na maamuzi juu ya eneo hilo.
Dkt Sengati ameomba eneo hilo kupatiwa muwekezaji atakayekuwa na uwezo kwa kuwa ni eneo zuri na linaweza kuifanya wilaya ya Magu mkoani Mwanza kubadilika kwa kiwango kikubwa.
Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya wilaya ya Magu Wlfred Mkono alisema eneo hilo lenye viwanja saba vyenye hati ya umiliki ardhi ya miaka 99 limerudishwa serikalini tangu April 25, 2019 na ofisi yake ilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha eneo hilo linakuwa katika mikono salama.