Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Uwekezaji Bi. Dorothy Mwaluko akizungumza wakati wa kikao cha Wadau wa Afya Moja walipokutana kujadili utekelezaji wa mpango mkakati wa afya moja nchini. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Uratibu Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bashiru Taratibu.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akielezea jambo kwa wadau wa Afya Moja walioshiriki kikao hiko kilichofanyika Hoteli ya Morena, Jijini Dodoma.
Mtaalamu Mshauri wa Afya Moja Dkt. Kunda John akichangia mada kuhusu umuhimu wa dhana ya Afya Moja wakati wa kikao kilichofanyika Julai 12, 2019 Jijini Dodoma.
Baadhi ya wataalamu wa Dawati la Afya Moja nchini wakifuatilia kwa makini maelezo ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Uwekezaji Bi. Dorothy Mwaluko (hayupo pichani) wakati wa kikao cha Wadau wa Afya Moja walipokutana kujadili utekelezaji wa mpango mkakati wa afya moja nchini.
Mratibu wa Dawati la Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Hansom Chinyuka akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Afya Moja nchini walipokutana Jijini Dodoma.
Sehemu ya wataalamu wa dawati la Afya Moja nchini wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Mratibu wa Dawati la Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Hansom Chinyuka (hayupo pichani).
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Uwekezaji Bi. Dorothy Mwaluko akiteta jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe mara baada ya kikao kilichowakutanisha na Wadau wa Afya Moja kwa lengo la kujadili utekelezaji wa mpango mkakati wa afya moja nchini.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
……………………
Na; MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko amewataka waratibu wa dawati la Afya Moja kutekeleza dhana ya Afya Moja kwa wakati sambamba na kuweka mikakati mahususi itakayowaongoza katika utendaji wa dhana hiyo.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha wadau wa afya moja na wataalam kutoka sekta ya Afya, Mifungo, Wanyamapori na Mazingira kilichofanyika Julai 12, 2019, Jijini Dodoma.
Alieleza kuwa dhana ya afya moja inajumuisha wataalam na wadau mbalimbali kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa dhana hiyo ikiwemo kutoa fursa ya kushirikiana pamoja katika kukabiliana na madhara au magojwa hatarishi nchini.
“Nimepitia Sera ya Afya moja na kuona suala hili linatakiwa kusimamiwa vyema, ikiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mratibu wa Dawati la Afya moja kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo, katika kuhakikisha nchi yetu inakuwa mahala salama,” alieleza Mwaluko
Aliongeza kuwa, suala la kujenga uwezo kwa waratibu wa dawati la afya moja inatakiwa kuangalia ofisi kwa ujumla na si mjumbe mmoja tu ambaye atakuwa anasimamia masuala hayo ya Afya moja wakati wote.
“Mnatakiwa mtambue kuwa mkiwa kama wafanyakazi mna majukumu mengine ya kiofisi ambayo mnatakiwa kuyatekeleza, hivyo mtoe fursa kwa wafanyakazi wengine waliopo kwenye ofisi zenu kujifunza na kuelewa dhana hii ya afya moja,” alieleza Mwaluko.
Aidha, alitoa wito kwa waratibu wa dawati hilo kuelimisha umma kuhusu maana ya Afya Moja na dhana nzima ya Afya moja ili wananchi waweze kuwa na ufahamu wa suala hilo.
Pia, aliwahimiza washauri elekezi wa dawati hilo kutimiza majukumu yao kwa weledi na kutoa ushauri mapema kuhusu dhana ya Afya Moja.
Kwa upande wake, Prof. Robinson Mdegela ambaye ni Mtaalamu Mshauri wa Afya Moja alisema kuwa kukutana kwao katika kikao hiko ni kuonesha utayari wa kila mtaalamu katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuongeza msukumo juu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Afya Moja.