Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Bashiru Ally akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya alipowasili kwenye ziara yake ya siku mbili.
Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru Ally akizungumza na viongozi wa mashina, matawi, kata na wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Manyara Simon Lulu na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia mkoa wa Manyara, Joachim Leonce.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akizungumza Mji mdogo wa Orkesumet juu ya maendeleo mbalimbali yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano.
************
KATIBU Mkuu wa CCM, Dkt Bashiru Ally amepongeza Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya kuwa ni mbunge mahiri, makini na mchapakazi ndiyo sababu wakakubali kumpokea CCM kwani waliwakataa wabunge watatu wa vyama vya upinzani waliiomba kujiunga na CCM baada ya kubaini kuwa hawawezi kukidhi vigezo vya kuwa wabunge wa chama hicho.
Dk Bashiru akizungumza Mji mdogo wa Orkesumet Wilayani Simanjiro kwenye ziara yake ya siku mbili Mkoani Manyara alisema Ole Millya ni miongoni mwa wabunge 10 mahiri waliokuwa upinzani wakakubaliwa kujiunga na CCM.
Alisema kwenye mkoa wa Manyara waliwapokea viongozi wawili wa upinzani Ole Millya na Pauline Gekul wa jimbo la Babati Mjini ambaye alikuwa mwanafunzi wake chuo kikuu.
Alisema CCM siyo chama cha kuchukua kila mtu ndiyo sababu wamewakataa hao ambao hakuwataja majina kwani wangewakubali kuwapokea wote upinzani ungemalizika.
“Tumewakataa wabunge hao watatu waliotaka kuja kwetu kwani CCM siyo jalala kwani mtu aliyekata tamaa anaweza kujiumiza mwenyewe au kuumiza wenzake,” alisema Bashiru.
Alisema siyo kweli kuwa wanafungua milango na kuchukua kila mtu kwani chama hicho cha CCM kina dhamira ya dhati na majukumu ya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza kwenye kikao hicho Ole Millya alisema miradi mingi ya maendeleo iliyofanyika Wilayani Simanjiro kupitia Rais John Magufuli ndiyo sababu yeye akajiuzulu Chadema na kujiunga na CCM.
Ole Millya alisema hivi sasa hospitali ya Wilaya inajengwa, mradi mkubwa wa maji wa mto Ruvu, barabara ya lami itajengwa kutoka Arusha hadi Kongwa Mkoani Dodoma kupitia Simanjiro na Kiteto na ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani.
Katika kikao hicho katibu mwenezi wa Chadema Wilayani Simanjiro na aliyegombea udiwani kata ya Orkesumet mwaka 2015, Zephania Kituyo alirudisha kadi ya Chadema na kujiunga CCM.
Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Manyara, Simon Lulu alisema hivi sasa majimbo yote saba ya mkoa huo yanaongozwa na wabunge wa CCM na Halmashauri zote saba zinaongozwa na wenyeviti kupitia CCM.
Katibu wa CCM wa wilaya ya Simanjiro Ally Kidunda alisema wamejipanga kuhakikisha mbunge na madiwani wa CCM wanafanya mikutano na wananchi na kuwasikiliza kero zao na kuzungumza nao.