Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma kwa Kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania [TCRA] kwa kanda ya kati limefanya Operesheni Maalum ya kuwasaka watu wanaojihusisha na usajili wa laini za simu bila idhini ya makampuni husika ya Simu na kukamata mawakala hewa 47 na laini za simu 4667..
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gillese Muroto amesema katika Msako huo umehusisha maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma yakiwemo Majengo,Sabasaba,Mipango,Nyerere Square,Sokoni,St.John , Chang,ombe ,Nanenane, na Nkuhungu,Bahi ambapo wamekamata wanaume 38 na wanawake 9 jumla yake 47.
Kamanda Muroto amesema katika Msako huo wamekamata vielelezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na laini za simu ambapo Vodacom 1300,tigo 1808,Airtel 716 ,Hallotel 694,TTCL 144 ikiwa ni jumla ya laini 4667 pamoja na simu 50 zilizokuwa zikitumika katika usajili huku pia jeshi hilo likibaini makosa ya kitambulisho kimoja kutumika kusajili laini zaidi ya Mtu mmoja ambapo ni makosa kisheria.
Hata hivyo,Kamanda Muroto ametoa wito kwa Waandishi wa Habari kuendelea kuelimisha jamii juu ya Masuala ya usajili ili wananchi waweze kuelewa juu ya mawakala matapeli wanaoweza kuiba nyaraka na taarifa muhimu za mawasiliano na utambuzi ikiwani pamoja na vitambulisho.
Kwa Upande wake Mwakilishi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania[TCRA]kanda ya kati amelishukuru jeshi hilo kwa ushirikiano huku akitoa wito kwa makampuni ya simu husika kukaa makini juu ya usajili wa laini za simu katika kupambana na wahalifu.
Msako huo ulilenga kukamata Mawakala wasio kuwa na barua rasmi kutoka kampuni husika ya simu,msajili alisiyekuwa na ofisi anuani na makazi ya Kudumu,asiyekuwa na leseni ya biashara au vitambulisho vya biashara vilivyotolewa na Rais John Pombe Magufuli.